1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya kuondolewa sehemu ya vikwazo vya silaha

17 Mei 2016

Marekani na nchi washirika zimesema zitaipatia silaha serikali ya Libya inayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa kulizuia kundi la Dola la Kiislamu, IS na makundi mengine ya wanamgambo kujiimarisha kwenye ardhi ya Libya.

https://p.dw.com/p/1IovC
Kushoto kwenda kulia, Waziri Mkuu wa Libya Fayaz al-Sarraj, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Paolo Gentiloni
Kushoto kwenda kulia, Waziri Mkuu wa Libya Fayaz al-Sarraj, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Paolo GentiloniPicha: Getty Images/D.Nagl

Hayo yamefikiwa katika mkutano uliomalizika usiku wa kuamkia leo mjini Vienna, Austria. Nchi hizo hizo leo hii zinaendelea na mazungumzo kuhusu mpango wa kumaliza vita nchini Syria.

Katika tangazo la pamoja baada ya mkutano huo wa Vienna, nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pamoja na nchi nyingine zaidi ya 15 zilizoshiriki katika mkutano huo, zimesema zitaridhia mauzo na misaada ya silaha kwa serikali mpya ya maridhiano ya kitaifa ya Libya.

Nchi hizo zimesema ziko tayari kuitikia wito wa serikali hiyo, ambayo imeomba msaada wa mafunzo na vifaa kwa vikosi vyake.

Waziri Mkuu wa Libya atoa rai

Waziri Mkuu anayeiongoza serikali hiyo Fayez al-Sarraj ambaye pia alikuwepo mjini Viena, ameeleza sababu za kuutaka msaada huo. ‘'Tumeomba tuondolewe vikwazo vya silaha, katika kuunga mkono jeshi na baraza la ofisi ya urais katika kupambana na IS'' amesema al-Sirraj, na kuongeza kuwa wameomba usaidizi katika kuandaa kikosi cha walinzi wa urais walichokiunda hivi karibuni.

Wanamgambo wa IS wamekita mizizi katika mji wa Sirte na maeneo yanayouzunguka
Wanamgambo wa IS wamekita mizizi katika mji wa Sirte na maeneo yanayouzungukaPicha: Getty Images/AFP/M.Turkia

''Kikosi hicho kina majukumu ya kulinda serikali na maeneo ya umma, sio kuchukua nafasi ya jeshi na polisi. Pia tumekubali kusaidia ukaguzi wa pwani katika kupunguza wahamiaji haramu.'' Amesisitiza kiongozi huyo.

Ukaguzi wa Pwani ya Libya ni miongoni mwa matakwa muhimu ya mataifa ya Umoja wa Ulaya yaliyoshiriki katika mkutano huo, ambayo yanatiwa hofu na mmiminiko mkubwa wa wahamiaji wanaoingia barani Ulaya wakipitia bahari ya Mediterania.

Wahamiaji wengi wameanza kuitumia njia hiyo, baada ya kufungwa kwa nyingine ilikuwa ikipitia Ugiriki na nchi za ukanda wa Balkan.

Changamoto ya kuweka mambo kwenye uzani

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amesema ingawa vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya Libya mwaka 2011 vitaendelea kuwepo, kuna haja ya kuisaidia serikali mpya ya maridhiano ya kitaifa nchini humo, ili iweze kutimiza majukumu yake na kutokomeza makundi ya wanajihadi.

Pwani ya Libya imekuwa uchochoro wa wahamiaji wanaoingia barani Ulaya
Pwani ya Libya imekuwa uchochoro wa wahamiaji wanaoingia barani UlayaPicha: DW/K. Zurutuza

Kerry amesema, ''Vikwazo vilivyopo vinairuhusu serikali ya maridhiano ya kitaifa kuomba silaha inazozihitaji kupambana na IS. Ni kitu kinachoeleweka, na tutatathmini maombi yote halali, huku tukizihimiza nchi zote kuimarisha vikwazo juu dhidi ya makundi yaliyo nje ya serikali hiyo, hapo kuna hali tete ya kuweka masuala hayo kwenye uzani.''

Hatua hizo zitaiwezesha serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa kuzilinda taasisi muhimu kama vile Benki Kuu na Shirika la Taifa la Mafuta. Lakini pia zinaendana na changamoto kubwa, hususan hofu kwamba silaha zitakazopelewa Libya zinaweza kuangukia mikononi mwa makundi ya wanamgambo.

Leo ni zamu ya Syria

Kabla ya mkutano huo kuanza, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alisema swali muhimu ni ikiwa Libya itaachiwa kuwa sehemu ambako magaidi na wasafirishaji haramu wa binadamu wanaendelea kupanua harakati zao, au kama jumuiya ya kimataifa kwa kushirikiana na serikali ya maridhiano ya kitaifa, wanaweza kurejesha utengamanao na umoja wa kitaifa.

Huko huko Vienna, yameanza leo mazungumzo kuhusu mpango wa kumaliza vita nchini Syria, na kufikisha msaada katika maeneo yaliyozingirwa. Waziri Steinmeier amesema mazungumzo hayo yanalenga kuwapa nguvu mpya mchakato wa mazungumzo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/afpe

Mhariri:Iddi Ssessanga