1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya mpya itafuata misimamo ya wastani ya Kiislamu

13 Septemba 2011

Viongozi wepya wa Libya wameahidi kuwa na utawala utakaofuata misimamo ya wastani ya Kiislamu huku Muammar Gaddafi akiapa kuendelea na vita kutoka mafichoni mpaka ushindi utakapopatikana.

https://p.dw.com/p/RlHr
Libyan Transitional National Council chairman Mustafa Abdel Jalil waves to Libyans as he delivers his speech in Martyr's Square in Tripoli, Libya, Monday, Sept. 12, 2011. The chief of Libya's former rebels arrived in Tripoli on Saturday, greeted by a boisterous red carpet ceremony meant to show he's taking charge of the interim government replacing the ousted regime of Moammar Gadhafi. (Foto:Francois Mori/AP/dapd)
Kiongozi wa Baraza la Kitaifa la Mpito, Mustafa Abdel JalilPicha: dapd

Kiongozi wa Baraza la Kitaifa la Mpito, Mustafa Abdel Jalil hapo jana alikaribishwa kwa shangwe kubwa katika mji mkuu wa Libya Tripoli, alipokwenda kuuhotubia umma uliokusanyika kwa maelfu kwenye uwanja mkuu. Ameuambia umati huo misimamo ya wastani ya Kiislamu ndio itakayokuwa kiini cha sheria za taifa jipya la Libya baada ya serikali ya Gaddafi kungolewa madarakani. Amesema, hawatokubali nadharia kali za mrengo wa kulia wala wa kushoto. Abdel-Jalil aliwasili Tripoli siku ya Jumamosi kwa mara ya kwanza tangu serikali ya Gaddafi kutimuliwa. Makamu wa Meya wa jiji la Tripoli Usama El-Abed alimkaribisha kwa kutamka hivi:

" Huu ni wakati wa kihistoria kwa taifa zima na sio kwa wakaazi wa Tripoli pekee. Kila mmoja amefurahi. Ninaamini kuwa ukurasa mpya umefunguliwa hivi punde katika mji huu wetu mkuu Tripoli."

Lakini kiongozi wa baraza la mpito la Libya,Mustafa Abdel Jalil alikumbusha kuwa taifa bado halijakombolewa. Alisema:

"Bado hatujakuwa huru, kwani Gaddafi ana fedha na dhahabu. Anaweza kuwanunua wapiganaji wepya. Tufahamu vizuri kuwa Gaddafi bado hajamalizika."

Former rebel fighters celebrate prior to heading to the frontline in Bani Walid, at a checkpoint between Tarhouna and Bani Walid, Libya, Saturday, Sept. 10, 2011. Libyan fighters are signing up for a final assault on one of the last remaining bastions of Moammar Gadhafi. The volunteers are pouring in by the dozens, coming in pickup trucks from cities as far as Tripoli and Tobruk, as a deadline expired on Saturday for the pro-Gadhafi loyalists holed up inside the town of Bani Walid to surrender. (Foto:Alexandre Meneghini/AP/dapd
Waasi wa zamani wakishangiria kabla ya kuelekea Bani WalidPicha: dapd

Wakati huo huo, vikosi vya Muammar Gaddafi kwa ghafula vimeshambulia upya kutoka pande tatu, huku Gaddafi akiapa kuwa ataendelea kupigana kutoka mafichoni mpaka ushindi utakapopatikana. Katika taarifa yake iliyosomwa kwenye stesheni ya televisheni ya Arrai Oruba iliyo na makao yake nchini Syria, Gaddafi amesema, haiwezekani kabisa kuitoa tena Libya kwa wakoloni. Hapo jana, vikosi vyake vilivyobakia vilishambulia mji wa Ras Lanuf wenye kiwanda cha kusafishia mafuta, mashariki ya nchi. Mapigano mengine yalitokea kwenye barabara inayoelekea mji wa Sirte, alikozaliwa Gaddafi na mji wa Bani Walid kusini-mashariki ya mji mkuu Tripoli. Lakini tangu vikosi vya Baraza la Mpito NTC kuuteka mji mkuu Tripoli, vikosi hivyo vimefanikiwa kusonga mbele kuelekea mji wa Sirte unaoadhibitiwa na wafuasi wa Gaddafi.

Wakati huo huo, ripoti iliyotolewa leo hii na shirika linalotetea haki za binadamu duniani, Amnesty International imeituhumu serikali ya Gaddafi kufanya uhalifu dhidi ya binadamu. Lakini ripoti hiyo pia inasema, wapiganaji wa NTC vile vile huenda walifanya uhalifu wa kivita. Kwa mujibu wa Amnesty International, katika siku za mwanzo za machafuko ya kuipinga serikali ya Gaddafi, makundi ya waandamanaji waliwaua wanajeshi waliokamatwa na hata watu walioshukiwa kuwa mamluki. Ripoti hiyo inasema,Baraza la Mpito linakabiliwa na changamoto kali ya kuwadhibiti wapiganaji wake na makundi ya sungusungu yanayohusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na huenda ikawa hata uhalifu wa kivita. Lakini baraza hilo halikuonyesha kuwa tayari kuchukua hatua za kuwawajibisha watu hao.

Mwanadishi:MartinPrema/afpe

Mhariri Abdul-Rahman