1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Livni ajaribu kuunganisha chama baada ya ushindi wake

P.Martin19 Septemba 2008

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert huenda akajiuzulu mapema juma lijalo. Kiongozi huyo,Jumapili anatazamiwa kuliarifu baraza la mawaziri na baadae kuwasilisha kwa rais barua ya kujiuzulu kwake.

https://p.dw.com/p/FLIf
**FILE** In this Sunday, Sept. 14, 2008 file photo, Kadima party leadership candidates, Israeli Transportation Minister Shaul Mofaz, left, and Israeli Foreign Minister Tzipi Livni, attend the weekly cabinet meeting in Jerusalem. Israel's popular foreign minister Tzipi Livni squares off against a tough-talking military man Shaul Mofaz on Wednesday when the ruling Kadima Party chooses a new leader to replace Prime Minister Ehud Olmert, who is being forced from office by a corruption scandal. (AP Photo/Dan Balilty, Pool, File)
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Tzipi Livni(kulia) aliemshinda Waziri wa Usafiri Shaul Mofaz kukiongoza chama cha Kadima.Picha: AP

Kuambatana na sheria ya Israel,kujiuzulu kwa Olmert kunaanza saa 48 baada ya kutoa barua yake.Kiongozi huyo anaeandamwa na shutuma za rushwa,alitangaza nia yake ya kujiuzulu tangu mwezi Julai.Na siku ya Jumatano,chama chake cha Kadima kilimchagua Waziri wa Mambo ya Nje Tzipi Livni kukiongoza chama hicho.Kwa mujibu wa sheria ya Israel,waziri mkuu anapojiuzulu,baraza la mawaziri pia halina budi kufanya hivyo na itakuwa serikali ya mpito.Na rais ana nafasi ya siku saba kumkabidhi kiongozi mwingine jukumu la kuunda serikali mpya.Kwa hivyo Livni,kiongozi mpya wa chama tawala cha Kadima atakuwa na siku 42 kuunda serikali mpya.Iwapo atashindwa,basi uchaguzi mpya utaitishwa katika kipindi cha siku 90 au mnamo mwezi Machi 2009,ikiwa ni mwaka mmoja mapema.

Lakini yadhihirika kuwa Livni atakuwa na kazi ngumu kupata washirika wa kutosha kuunda serikali yenye wingi bungeni ili aweze kujiepusha na uchaguzi wa mapema.Kwani ishara za mwanzo za mvutano katika chama chake cha Kadima zilidhihirika saa chache baada ya kumshinda Waziri wa Usafiri Shaul Mofaz kwa wingi mdogo wa asili mia 1.1 tu yaani kwa kura 431.Muda mfupi baadae Mofaz akatangaza kuwa kwa muda ataachana na shughuli za kisiasa,huku viongozi waandamizi katika chama chake cha Kadima wakisema uamuzi huo ni pigo kwa chama.Hii leo Waziri Livni katika juhudi ya kurejesha umoja katika chama tawala cha Kadima ameitisha mkutano wa wanachama waandalizi.Amesema, amesikitishwa na uamzi wa Mofaz.Na wasaidizi wa Livni walimuomba Mofaz afikirie upya uamuzi wake lakini amekataa kukutana na Livni na wala hakuhudhuria mkutano wa hii leo.Vyombo vya habari vinahisi kuwa Mofaz mwenye sera za kihafidhina huenda akarejea kwenye chama cha upinzani cha mrengo wa kulia-Likud Party.Kwani ni katika mwaka 2005 Mofaz,Livni na Olmert walijitoa kwenye chama hicho na wakaunda chama kipya cha Kadima.

Ni dhahiri kuwa mjasusi wa zamani wa Mossad Bibi Livni,mwenye miaka 50 atakuwa na kazi ngumu kuunda serikali mpya.Kwa mujibu wa gazeti la Yediot Aharonot,chama cha Labour chenye siasa za wastani za mrengo wa kushoto-mshirika mkuu katika serikali ya mseto ya Olmert-kinataka uchaguzi uitishwe haraka.Katika kinganyiro hicho cha madaraka,chama kitakachonufaika iwapo kutaitishwa uchaguzi wa mapema,ni chama cha upinzani cha Likud kinachoongozwa na Benjamin Netenyahu mwenye siasa kali za mrengo wa kulia.Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa chama hicho kitatokeza kama chama kikuu na hivyo kiongozi wake Benjamin Netanyahu aliewahi kuwa waziri mkuu,ndio atakaepewa jukumu la kuunda serikali.Netanyahu ameutumia ushindi mdogo wa Livni kudai uchaguzi wa mapema.