1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Livni ataka uchaguzi uitishwe mapema Israel

S.Engelbrecht - (P.Martin)27 Oktoba 2008

Nchini Israel chama tawala Kadima kimewasilisha mswada wa kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mapema,baada ya kiongozi wa chama hicho Tzipi Livni kutokuwa tayari kuridhia masharti makali ya chama cha kidini cha Shas.

https://p.dw.com/p/FheD
Israeli Foreign Minister Tzipi Livni attends the Israeli Foreign Ministry's Conference for Policy and Strategy at the Israeli Foreign Ministry in Jerusalem, October 5, 2008. Foreign Minister Tzipi Livni said that she will continue the peace negotiations with the Palestinians as leader of the Kadima Party. UPI Photo /Landov +++(c) dpa - Report+++
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Tzipi Livni.Picha: picture-alliance/ dpa

Uamuzi huo umesifiwa lakini kinachoulizwa ni iwapo chama chake kitaweza kushinda uchaguzi ulioitishwa kufanywa kabla ya wakati wake.

Septemba 22 Rais wa Israel Shimon Peres alimpa Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Tzipi Livni jukumu la kuunda serikali mpya kuchukua nafasi ya serikali iliyokuwa ikiongozwa na Ehud Olmert aliejiuzulu ili awe na nafasi ya kujitetea dhidi ya mashtaka ya rushwa yanayomkabili.Lakini siku ya Jumapili,Livni alie pia kiongozi wa chama cha Kadima alitangaza kuwa hakufanikiwa kuunda serikali mpya na akamuomba Rais Peres kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Livni ameungwa mkono na chama cha Labour kinachoongozwa na waziri mkuu wa zamani Ehud Barak lakini hakuweza kukubaliana na masharti ya chama cha Shas chenye sera kali za kidini.Livni alipinga madai ya Shas kinlichotaka Euro milioni 200 ziada kwa malipo ya watoto.Livni alikuwa tayari kutoa milioni 120 na si zaidi ya hapo.Vile vile hakuwa tayari kuridhia dai la chama cha Shas kuahidi kutolijadili suala la Jerusalem katika mazungumzo ya amani pamoja na Wapalestina.Kwa maoni ya Israel,mji mzima wa Jerusalem ni mji mkuu wao usioweza kugawanywa.Lakini Wapalestina wanaitaka sehemu ya mashariki ya Jerusalem kuwa mji mkuu wa taifa la Palestina litakaloundwa katika siku zijazo.Livni anataka kuwa waziri mkuu wa Israel lakini,bila ya kusaliti msimamo wake wa kisiasa.

Majuma matano yaliyopita alipochaguliwa kukiongoza chama chake cha Kadima,Livni aliahidi kuanzisha sera mpya za kisiasa.Sasa Waisraeli wanaelewa kile alichomaanisha,kwani amechomoza kama mwanasiasa anaesimama imara kwenye misingi anayoamini kwa manufaa ya kisiasa ya taifa.Livni anaamini msimamo huo utamsaidia katika uchaguzi ujao na yeye wala hana hofu ya kukabiliana na mpinzani wake mkuu Benjamin Netanyahu anaekiongoza chama cha kihafidhina cha Likud.Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na magazeti mawili nchini Israel,chama tawala cha Kadima kitaweza kukishinda kwa wingi mdogo, chama kikuu cha upinzani Likud,iwapo uchaguzi utaitishwa mapema mwakani.