1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Loew aweka imani kwa wachezaji wenye uzoefu

Bruce Amani
7 Septemba 2018

Ujerumani inajaribu kuhamia enzi mpya baada ya kampeni mbovu ya Kombe la Dunia, lakini sare yao ya 0-0 dhidi ya Ufaransa imeonyesha umuhimu wa kocha Joachim Loew wa kuwaamini wachezaji wa muda mrefu

https://p.dw.com/p/34VKy
Fußball Nations League München Deutschland vs Frankreich
Picha: Imago/Matthias Koch

Kikosi cha kwanza cha Loew katika uwanja wa Allianz Arena dhidi ya mabingwa wa dunia kilikuwa na wachezaji wanne wa timu ya Ujerumani iliyoifunga Argentina katika fainali ya Kombe la Dunia 2014 – mlinda mlango Manuel Neuer, mabeki Mats Hummels na Jerome Boateng, kiungo Toni Kroos na mshambuliaji Thomas Mueller-

Wachezaji hao wanne, ambao wameichezea timu ya taifa mara 400 baina yao, walikuwa nguzo ya timu ambayo ingefanikiwa kuilaza Ufaransa kama sio kazi safi sana aliyofanya kipa wa Les Bleus Alphonse Areola, hasa kutoka kwa mashambulizi Ya Marco Reus, Mueller na kisha Mathias Ginter katika kipindi cha pili.

Kikosi kizima cha Ujerumani kilichoanza mechi hiyo yao ya ufunguzi ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya kilikuwa sehemu ya timu iliyocheza Urusi, wakati ilipobanduliwa nje katika hatua ya makundi.

Fußball Nations League München Deutschland vs Frankreich
Ujerumani iliwatuliza mabingwa wa dunia UfaransaPicha: Reuters/M. Dalder

Sura iliyobadilika pekee ni ya Leroy Sane, winga wa Manchester City aliyeingia kama nguvu mpya baada ya kuwachwa nje katika kikosi cha wachezaji 23 waliokwenda Urusi. Wachezaji kama vile Thilo Keher na Kai Havertz walibaki kwenye benchi. Loew alisema bila shaka ni wakati wa kuwashirikisha wachezaji wapya. Lakini akakiri kuwa ni mchakato wa muda mrefu ambao hautafanikiwa haraka

Kwamba dhidi ya Ufaransa, wachezaji kama vile Hummels, Boateng na Kroos walikuwa muhimu sana, kwa sababu ya ujuzi wao, uzoefu, na ubora wao.

Loew pia aliamua kuanza na Ginter na Antonio Ruediger, ambao kawaida huwa mabeki wa kati, na kuwaweka katika nafasi za kuwa mabeki wa kupanda na kushuka, uamuzi ambao ulizaa matunda kwa sababu Ujerumani iliwanyamazisha Kylian Mbappe, Antonio Griezmann na wengine.

Kroos alisema ilisikitisha kuwa Ujerumani hawakufunga bao. Lakini walitaka kuwa na ulinzi mzuri baada ya kile kilichotokea katika Kombe la Dunia. Lilikuwa kipau mbele na anadhani walifaulu katika hilo

Ujerumani ambao watawaalika Peru siku ya Jumamosi mjini Sinsheim, wanatumai kusahau yaliyowakumba katika Kombe la Dunia la Urusi. Hali iliyogubikwa na uamuzi wa Mesut Özil kustaafu kutoka kandanda la kimataifa kutokana na madai ya ubaguzi wa rangi yaliyoelekezwa kwa rais wa kandanda Shirikisho la Kandanda la Ujerumani – DFB, Reihnard Grindel.

Loew alisaini mkataba mpya wa hadi mwaka wa 2022 kabla ya kuanza Kombe la Dunia, na Ligi ya Mataifa ya Ulaya inampa fursa ya mapema ya kuwaleta pamoja mashabiki kwa mara nyingine. Ujerumani itachuana na Uholanzi na Ufaransa ugenini mwezi Oktoba, ambapo mshindi wa kundi lao atafuzu katika fainali za timu nne za Ligi ya Mataifa Juni mwaka ujao.

Mwandishi: Bruce Amani

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman