1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON: Shirika la ujasusi la Uingereza lakabiliwa na shinikizo

1 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC5X

Kufuatia uamuzi wa mahakama kuwahukumu Waingereza watano kifungo cha maisha gerezani hapo jana, shirika la ujasusi la MI 5 linakabiliwa na mbinyo mkubwa kwa madai kwamba lingeweza kufanya mengi zaidi kuzuia mashambulio ya mabonu ya Julai saba mnamo mwaka wa 2005 mjini London.

Jopo la wabunge watano wa Uingereza linachunguza kwa nini shirika la ujasusi la MI5 lilivoyoshindwa kuwatia mbaroni washambuliaji wa kujitoa mhanga maisha, licha ya kwamba lilikuwa likiwachunguza washukiwa hao kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya mashambulio hayo.

Jamii za wahanga wa mashambulio hayo zimekasirika na zinataka viongozi wa upinzani nchini Uingereza waitishe tume huru kuchunguza kadhia hiyo.

Sambamba na taarifa hizo, waziri mkuu wa Uingereza, Tony Blair, amesema atatangaza juma lijalo lini atakapojiuzulu kutoka kwa wadhifa wake.

Blair ameyasema hayo leo asubuhi wakati wa mahojiano na runinga moja mjini London, miaka kumi tangu chama cha Labour kiliposhinda uchaguzi mkuu na kuingia madarakani nchini Uingereza.

Waziri mkuu Blair amemsifu mrithi wake waziri wa fedha, Gordon Brown, akisema atakuwa kiongozi mahiri.