1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lukashenko yuko Urusi kwa mazungumzo na Putin

Saumu Mwasimba
14 Septemba 2020

Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko yuko Belarus ambapo anakutana na rais Vladmir Putin kutafuta uungwaji mkono wa serikali ya Urusi baada ya kuendelea kukabiliwa na maandamano makubwa ya umma nchini mwake

https://p.dw.com/p/3iR4V
Russland Sotschi Ankunft Präsident von Belarus Alexander Lukaschenko
Picha: Reuters/BelTA/A. Stasevich

Rais huyo wa Belarus anakabiliwa na shinikizo la umma unaomtaka na sasa hatma yake iko mikononi mwa rais Vladmir Putin aliyekwenda kukutana nae kwenye mji wa kitalii wa Sochi.

Alexander Lukasheno anakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi ambao hajapata kuushuhudia katika kipindi chake chote cha miaka 26 madarakani nchini Belarus.Msaada wa kiuchumi na kijeshi kutoka mjini Moscow huenda ukasaidia kumpa nguvu wakati vikosi vyake vya usalama vikiendelea kuwaandama wapinzani. Soma pia: Tikhanovskaya: Lukashenko sio rais halali machoni mwa wabelarus

Upinzani nchini humo unamshutumu Lukashenko kwa wizi wa kura katika uchaguzi wa rais wa mwezi uliopita ambao anasema alishinda kwa haki kabisa asilimia 80 ya kura. Tangu wakati huo maelfu ya wabelarus wamekamatwa na kiasi viongozi wote wa upinzani wamekamatwa ,kuondolewa Belarusau kulazimika kuikimbia nchi hiyo.

Belarus Minsk | Proteste & Verhaftungen
Waandamanaji 400 wakamatwa BelarusPicha: picture-alliance/Tass/V. Sharifulin

Jana Jumapili kiasi waandamanaji laki moja waliingia mitaani katika mji mkuu Minsk wakiandamana huku wakisikika wakimwita Lukashenko kuwa panya. Polisi waliwakamata watu 774 katika maandamano katika sehemu mbali mbali za nchi.

Vitendo vya rais Wladmir putin wa Urusi vinaonesha kwamba hana nia ya kumuona kiongozi huyo wa nchi jirani yake iliyowahi kuwa sehemu ya muungano wa kisovieti akiondolewa madarakani kwa nguvu ya umma,licha ya kwamba Lukashenko mara kadhaa amedhihirisha wazi kwamba sio mshirika mwepesi. Soma pia: Belarus: Lukashenko asema haondoki ng'o madarakani

Itakumbukwa kwamba hata mwezi uliopita rais huyo wa Urusi alitangaza kwamba ameshaandaa kikosi cha akiba cha jeshi la polisi kwa ajili ya kumsaidia Lukashenko lakini kikosi hicho kitatumwa Belarus ikiwa tu itahitajika.

Shirika la habari la urusi RIA likiinukuu wizara ya ulinzi ya nchi hiyo limeripoti kwamba Urusi leo jumatatu itapeleka wanajeshi wa miamvuli nchini Belarus kushiriki kwenye operesheni ya mazoezi ya kijeshi yatakayoendelea hadi tarehe 25 mwezi huu wa Septemba.Kadhalika Urusi imejitolea kuirahisishia ulipaji wa madeni pamoja na kuusaidia mfumo wake wa benki. Soma pia: Belarus:Kiongozi wa upinzani akamatwa katika mpaka na Ukraine

Belarus ni mshirika wa karibu sana wa kisiasa,kijamii kiuchumi na kiulinzi na Urusi,lakini gharama za Belarus kupata uungaji mkono zaidi kutoka Urusi huenda ikawa ni hatua ya Lukashenko kuridhia Urusi kuwa na usemi zaidi ndani ya taifa hilo.

Wakati huohuo jana kiongozi mkuu wa kanisa katoliki mjini Vatican Papa Francis aliwataka viongozi wa kisiasa kuwasikiliza waandamanaji na kuleta mabadiliko ya kisiasa na kijamii yanayoliliwa na waandamanaji. Kauli hiyo ya Papa ingawa haikuitaka moja kwa moja Belarus au nchi nyingine yoyote lakini ilionesha kuilenga nchi hiyo.

afp, dpa, ap, reuters