1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LUXEMBOURG: Umoja wa Ulaya kuisaidia serikali mpya ya Palestina

18 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBqg

Umoja wa Ulaya umesema utaanza kupeleka misaada ya moja kwa moja kwa serikali mpya ya mpito ya mamlaka ya Palestina.

Kiongozi anayehusika na sera za kigeni wa umoja huo, Javier Solana, amesema umoja wa Ulaya utatafuta njia za kupeleka misaada katika Ukanda wa Gaza na utaishawishi Israel ianze kutoa fedha inazozizuilia kama ushuru wa Palestina.

Umoja wa Ulaya ulisitisha misada kwa serikali ya mamlaka ya Palestina mnamo mwezi Machi mwaka jana wakati serikali inayoongozwa na chama cha Hamas ilipoingia madarakani katika maeneo ya Wapalestina.

Serikali mpya ya Palestina imekutana kwa mara ya kwanza bila wajumbe wa chama cha Hamas mjini Ramallah mapema leo. Mkutano huo umeongozwa na waziri mkuu mpya, Salam Fayyad.

Sambamba na hayo, waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, ameonya kwamba mzozo juu ya kuifufua katiba ya Ulaya huenda ukautatiza mkutano wa umoja wa Ulaya utakaofanyika wiki hii mjini Brussels, Ubelgiji.

Waziri Steinmeier amesema hakuna uhakika ikiwa mkutano huo utafaulu.

Poland imetishia kutumia kura yake ya turufu kuitilia guu katiba ya Ulaya ikiwa mabadiliko hayatafanywa kwenye katiba iliyopendekezwa.