1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafa yaongezeka Gaza

13 Julai 2014

Israel imeendeleza mashambulizi ya anga na mizinga dhidi ya Gaza kwa siku ya tano mfululizo Jumamosi (12.07.2014) na kuuwa Wapalestina 22 wakati Hamas nayo ikiendelea kuvurumisha maroketi yake nchini Israel.

https://p.dw.com/p/1CboA
Kifusi cha msikiti ulioshambuliwa huko Nuseirat katikati ya Ukanda wa Gaza. ((12.07.2014)
Kifusi cha msikiti ulioshambuliwa huko Nuseirat katikati ya Ukanda wa Gaza. ((12.07.2014)Picha: REUTERS

Pande zote mbili zimepuuza wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano na Israel imeendelea kukusanya vikosi vyake na magari ya kivita kwenye mpaka na Gaza kwa ajili ya kujiandaa na uwezekano wa kuivamia Gaza kwa kutumia majeshi ya ardhini.

Mashambulizi ya Jumamosi ambayo wahudumu wa dharura huko Gaza wamesema yamepiga misikiti miwili na kituo cha walemavu miongoni mwa maeneo mengine yaliyolengwa,yamefanya idadi ya vifo tokea kuanza kwa operesheni hiyo ya mashambulizi ya Israel hapo Jumanne kufikia 127.

Jeshi la Israel limesema mmojawapo wa msikiti ulikuwa umetumika kuficha hazina ya silaha na kwamba katika kipindi hicho maroketi 530 yamerushwa Israel na kwamba tisa kati yao yamevurumishwa Jumamosi. Rais Barack Obama wa Marekani hapo Ijumaa alizungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na kupendekeza kutumia ushawishi wa serikali yake Mashariki ya Kati kurudisha utulivu katika eneo hilo.

Mzozo wapamba moto

Akizungumza na waadishi wa habari mjini Tel Aviv Ijumaa hiyo hiyo Netanyahu amesema hakuna shinikizo la kimataifa litakalowazuwiya kushambulia kwa nguvu zote makundi ya kigaidi yanayotowa wito wa kungamizwa kwa Israel.

Rais Abdel Fattah al -Sisi wa Misri ameonya Jumamosi kwamba mzozo huo kati ya Israel na Wapalestina unaozidi kupamba moto utazidi kugharimu maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

Mjumbe wa mzozo wa Mashariki ya Kati Tony Blair (kushoto) na Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri mjini Cairo . (12.07.2014)
Mjumbe wa mzozo wa Mashariki ya Kati Tony Blair (kushoto) na Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri mjini Cairo . (12.07.2014)Picha: picture-alliance/dpa

Msemaji wa rais huyo amesema serikali inawasiliana na pande zote mbili kufuatia mkutano wa Sisi na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Ton Blair mjumbe wa kundi la pande nne lenye kushuguhulikia mzozo wa Mashariki ya Kati ambaye amewasili Cairo kushinikiza kukomeshwa kwa umwagaji damu huo.

Ismail Haniya waziri mkuu wa zamani wa Ukanda wa Gaza na afisa mwandamizi wa kundi la Hamas katika ukanda huo wa mwambao amefuta uwezekano wa kusitishwa uhasama.Amesema Israel ndio ilioanza uvamizi huo na lazima iache kufanya hivyo kwa sababu wanachofanya Wapalestina ni kujihami tu.

Mashambulizi ya ardhini

Israel imesema maandalizi yanaendelea kufanyika kwa uwezekano wa uvamizi wa ardhini kwa kutumia vifaru na vikosi vilivyokusanywa kwenye mpaka na Gaza na kikosi cha akiba cha wanjeshi 33,000 kati ya 40,000 kilichoidhinishwa na baraza la mawaziri. Magari zaidi ya kivita yameonekana yakielekea upande wa kusini wa Israel Jumamosi asubuhi.

Kikosi cha mizinga cha Israel nje ya eneo la Gaza ya Kati.(12.07.2014)
Kikosi cha mizinga cha Israel nje ya eneo la Gaza ya Kati.(12.07.2014)Picha: Reuters

Waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman amesema anataraji uamuzi wa kisiasa juu ya uwezekano wa kufanya operesheni hiyo ya ardhini utatolewa Jumapili. Amesema kinachofanyika hivi sasa ni awamu ya kwanza ya mashambulizi ya anga. Kuwait imeomba kufanyika kwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu kujadili hali inayozidi kuwa mbaya ambapo mwanadiplomasia katika Jumuiya ya Waarabu amesema utafanyika Jumatatu.

Mashambulizi ya anga ya Israel kwenye majengo ya wakaazi huko Gaza yamekabiliwa na karipio kutoka ofisi ya masuala ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na maafa ya raia.Msemaji wa ofisi hiyo Ravina Shamdasani amesema hata kama nyumba inatambuliwa kuwa inatumika kwa dhamira za kijeshi shambulio lolote linapaswa kuwa la kiasi na tahadhari lazima zichukuliwe kuwalinda raia.

Vikwazo vya silaha

Shirika la haki za binaadamu la kimataifa Amnesty International limeutaka Umoja wa Mataifa kuweka mara moja vikwazo kabambe vya silaha dhidi ya Israel,Hamas na makundi ya wapiganaji ya Kipalestina na kuanzisha uchunguzi kwa ukiukaji wa haki za binaadamu uliofanywa na pande zote.

Waombolezaji wa wanamgambo wa Kipalestina aliyeuwawa na mashambulizi ya Israel wakati wa mazishi yake Gaza.(12.07.2014)
Waombolezaji wa wanamgambo wa Kipalestina aliyeuwawa na mashambulizi ya Israel wakati wa mazishi yake Gaza.(12.07.2014)Picha: REUTERS

Mzozo huo wa sasa ambao ni mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa tokea mwezi wa Novemba mwaka 2012 chanzo chake ni kutekwa nyara na kuuwawa kwa vijana watatu wa Israel katika eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel la Ukingo wa Magharibi mwezi uliopita na kisasi cha kuuwawa kinyama kwa kijana wa Kipalestina kilichofanywa na Wayahudi wa misimamo mikali.

Israel ilifanya msako mkubwa dhidi ya Hamas licha ya kwamba kundi hilo la itikadi kali la Kiislam limekataa kuthibitisha au kukanusha kuhusika na mauaji ya vijana wa Israel,wakati wanamgambo wa Gaza walijibu mapigo kwa kuvurumisha maroketi mfululizo nchini Israel. Hadi sasa hakuna Muisrael aliyeuwawa lakini wawili wamejeruhiwa vibaya sana.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP/

Mhariri : Amina Mjahid