1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa wa UN waanza ziara Djibouti kubaini hali halisi

Reuben Kyama3 Oktoba 2019

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameiomba jumuia ya kimataifa kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaokimbilia Djibouti.

https://p.dw.com/p/3QgYK
Dschibuti Flüchtlinge
Picha: DW/A. Stahl

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Naibu Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Ursula Mueller ameanza ziara rasmi ya siku tatu nchini Djibouti ili kubaini hali halisi ya mahitaji ya kibinadamu kwa maelfu ya wakimbizi wanaomiminika katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameiomba jumuia ya kimataifa kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa lengo la kuisaidia idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanaokimbilia Djibouti kutokana na misukosuko ya kivita na majanga mbalimbali.

''Ongezeko kubwa la idadi ya wakimbizi na wahamiaji duniani ina athari ya moja kwa moja kwa nchi ya Djibouti. Kwa sasa nchi hiyo inawahifadhi zaidi ya wakimbizi na wahamiaji 30,000 nusu yao wakiwa ni watoto kutoka Somalia, Ethiopia, Eritrea na Yemen. Hali inaongeza mahitaji ya misaada ya kibinadamu''. Ursula amesema.

Aidha amekutana na kufanya mashauriano ya ana kwa ana na Waziri Mkuu wa Djibouti, Abdulkadir Kamil Mohammed.

Akizungumza na idhaa ya DW punde tu baada ya mazungumzo hayo, Bi Mueller, ambaye ni raia wa Ujerumani, amesifu juhudi za serikali ya Djibouti za kuwasaidia maelfu ya wakimbizi na wahamiaji wanaokimbilia nchini humo.

Naibu Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Ursula Mueller
Naibu Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Ursula MuellerPicha: picture-alliance/dpa

Ursula amesema ''Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu yanaendeleza kutoa msaada nchini humu, na mapema mwaka huu Shirika la Umoja wa Mataifa limetenga dola milioni 4 kwa ajili ya kutoa misaada ya dharura ya kibinadamu nchini Djibouti. Ufadhili huo umeleta mabadiliko na mafanikio makubwa kwa maisha ya watu wanaokabiliwa na hali gumu''.

Kadhalika mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amehimiza jumuiya ya kimataifa kuzidisha misaada ya kiutu ili kushughulikia majanga na tatizo la ukosefu wa chakula na maji.

Wakati wa ziara yake hiyo, Bi Mueller anadhamiria kujionea hali halisi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa nchi za Pembe ya Afrika na kutathmini mahitaji ya misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi na wahamiaji. Ursula ameongeza kuwa ''Na ndiyo sababu naihimiza jumuia ya kimataifa kuzidi kusaidia operesheni za kutoa misaada nchini Djibouti''.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa theluthi moja ya idadi ya raia nchini Djibouti, sawa na zaidi ya watu 280,000 wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula. Isitoshe, Djibouti pia inatoa hifadhi kwa raia wa kigeni wapatao 30,000 ambao ni wakimbizi na wahamiaji waliokimbia makwao kutokana na migogoro ya kivita.

Naibu huyo mkuu wa OCHA, anatarajiwa kuhitimisha ziara yake nchini humo hapo kesho siku ya Ijumaa.