1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maambukizi ya corona yaongezeka duniani

30 Desemba 2021

Wakati maambukizi ya virusi vya Omicron yakiendelea kuongezeka duniani, nchi mbalimbali zimechukua hatua za kukabiliana na ongezeko hilo huku baadhi ya matatizo yakidhihirika.

https://p.dw.com/p/450IV
Coronavirus Rostock | Patienten auf der Intensivstation
Picha: Jens Büttner/dpa/picture alliance

Wakaazi na watalii huko mjini Paris nchini Ufaransa watalazimika kuvaa barakoa wakiwa nje kuanzia Ijumaa hii wakati nchi hiyo sambamba na mataifa mengine ya Ulaya yakishuhudia kuongezeka kwa maambukizi ya COVID-19 yanayochochewa na kirusi Omicron. 

Mamlaka ya mji wa Paris imesema sheria hiyo ya barakoa itawahusu watu wenye umri wa miaka 12 na zaidi, ispokuwa wale watakaokuwa wakiendesha baiskeli au pikipiki, kusafiri kwa magari yao binafsi na kufanya mazoezi. Watakaokiuka sheria hizo wanakabiliwa na faini ya euro 135  sawa na dola za kimarekani 153.

Amri ya uvaaji wa barakoa tayari inatekelezwa katika maduka, usafiri, ofisi na majengo ya umma. Serikali ya Ufaransa imetangaza hatua hizo wiki hii, wakati Ufaransa ilishuhudia zaidi ya visa 208,000  vya COVID-19 siku ya Jumatano. 

Vizuizi vipya nchini Italia, China na Saudi Arabia

Serikali ya Italia imetilia mkazo sheria zake za kupambana na covid na wakati huo huo wakilegeza hatua za karantini. Kuanzia Januari 10, watu ambao hawajachanjwa hawatoruhusiwa kwenye mahoteli, makumbi ya mikutano, usafiri wa umma wa ndani na wa umbali mrefu, kutumia vigari kwenye michezo ya kuteleza kwenye theluji, na hata kuhudhuria matamasha mbalimbali. Hizo ni miongoni mwa hatua zilizo chukuliwa usiku wa kuamkia Alhamisi na mamlaka mjini Roma.

Symbolbild I Flugausfall I Flughafen
Baadhi ya wasafiri wakiwa wanatafakari baada ya safari kadhaa za ndege kufutwaPicha: Rebecca Blackwell/AP/picture alliance

Na huko nchini China katika mji wa Xi´an uliopo kwenye vizuizi vikali, Wakaazi wamesema wanatatizika kupata lishe kamilifu, licha ya Beijing kusisitiza Alhamisi kwamba sasa kuna vyakula vya kutosha. 

Serikali ya china imefuata mbinu madhubuti ya "sifuri Covid" inayojumuisha vizuizi vikali vya mipakani na kufungwa kwa shughuli za umma haraka tangu virusi hivyo vilipoibuka katika katika mji huo mkuu mwishoni mwa mwaka 2019. Wakaazi wote milioni 13 wa Xi'an wamewekwa chini ya vizuizi siku nane zilizopita, na maafisa wa eneo hilo wamekiri kwamba kumekuwa na shida ya upatikanaji wa vifaa muhimu. 

Hatua mpya Saudia

Nayo Saudi Arabia imerejesha Alhamisi hii hatua za kukabiliana na virusi vya corona katika mji mtakatifu wa Waislamu wa Makkah, baada ya kushuhudia idadi kubwa zaidi ya maambukizo katika miezi ya hivi karibuni. 

Ufalme huo wenye takriban watu milioni 34 hadi sasa umerekodi zaidi ya visa 554,000 vya covid, pamoja na vifo 8,874, ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya vifo katika nchi za Ghuba. Janga la Covid-19 limevuruga kwa kiasi kikubwa shughuli za mahujaji wa Kiislamu, ambao kwa kawaida ni waingizaji mapato muhimu kwa Falme hiyo, na huleta takriban dola bilioni 12 kila mwaka. 

Vyanzo: AFP, DPA, Reuters