1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandalizi ya kabla ya kuanza Bundesliga

Sekione Kitojo
10 Julai 2017

Vilabu 18 vya ligi daraja la kwanza Ujerumani Bundesliga vimeanza rasmi maandalizi ya msimu wa mwaka 2017 - 18 ambao ni wa 55 tangu kaunzishwa kwa ligi hiyo mnamo mwaka 1963

https://p.dw.com/p/2gI2x
1. Bundesliga - FC Bayern München Muenchen - BVB Borussia Dortmund: Ousmane Dembele & Christian Pulisic
Wachezaji Ousmane Dembele na Christian Pulisic wa Borussia Dortmund Picha: picture-alliance/augenklick/firo Sportphoto/S. el-Saqqa

Klabu  ya  mwisho  kujiunga  na  vilabu vingine  katika  maandalizi  hayo  ni  Borussia  Dortmund ambayo ilifanya  hivyo tarehe 7 Ijumaa  mwezi  huu, wakati vilabu  vingine  tayari  vilianza  mchakato  huo katikati  ya mwezi  uliopita.

Antonio Rüdiger, deutscher Fußballspieler
Antonio Ruediger ambaye anajiunga na Chelsea msimu ujaoPicha: picture-alliance/Pressefoto Ulmer/M. Ulmer

Mbali  na  maandalizi  hayo  pia  kuna  heka  heka  ya  nani anajiunga  na  timu  gani  na  nani  anahamia kwingine. Kwa  kuwa dirisha  la  usajili halijafungwa  hadi  mwezi  wa nane , bado  kuna  tetesi  za  hapa  na  pale  za  wachezaji kuzihama  timu  zao  kutafuta  malisho  bora  zaidi na  pia kutafuta  maeneo  ya  kujulikana na kuongeza kiwango chao zaidi.

Antonio Rudiger mchezaji  wa  timu  ya  taifa  ya Ujerumani  na  bingwa  wa  kombe  la  mabara, Confed Cup, anahamia  Chelsea  katika  ligi  ya  England  ambapo inasemekana  kocha  mkuu  wa  timu  hiyo  Antonio Conte anapanga  msimu  ujao kuichezesha  timu yake kwa mfumo  wa  3-4-3, ambapo ulinzi  wa  timu  hiyo  utakuwa na  wachezaji  watatu  pamoja  na  David Luiz, Gary Cahill na  Antonio Rudiger.

Mfumo  huo ulitumika  sana  msimu uliopita  na  timu  za  Ujerumani, kama  vile 1899 Hoffenheim na  ukaifikisha  timu  hiyo  kucheza  ligi ya mabingwa  Ulaya , Champions league  msimu  ujao, Schalke 04, na  mahasimu  wao  wakubwa  Borussia Dortmund  ambao  walitumia  mtindo  huo mara chache wanapoona kuna  ulazima.

1. FC Köln - Borussia Dortmund | Pierre Aubameyang & Anthony Modeste
Pierre Emerick Aubameyang (kushoto) na Anthony Modeste (kulia)Picha: picture-alliance/Gladys Chai von der Laage

Anthony Modeste  mwenye  umri  wa  miaka  29 na ambaye  msimu  uliopita  alichuana vikali  na  wakali  kama Robert Lewandowski  (Bayern Munich)na  bingwa wa mtutu  wa  bunduki  Pierre Emerick Aubameyang  wa Borussia  Dortmund  katika  kuwania  mtutu  huo, alifanikiwa  kupachika  mabao 25  kwa  FC Kolon  na kuisaidia  timu  hiyo  kufikia  kucheza   ligi  ya  Ulaya   kwa mara  ya  kwanza  katika  muda  wa  miaka zaidi  ya 25,lakini  ameamua  kuipa  kisogo  timu  hiyo  na  kwenda katika  klabu  ya  Tianjian Quanjian  ya  China.

Pia  ligi  ya  Ujerumani  itamkosa Philipp Lahm , Xabi Alonso  ambao  wametundika  madaluga yao, Douglas Costa wote wa  Bayern Munich anahamia  Juventus Turin kwa  mkopo licha ya kwamba mazungumzo kuhusu uhamisho bado yanaendelea.

Ligi  inaanza  tarehe  18  Agosti.

Bundesliga Spielervorstellung bei Borussia Mönchengladbach | Matthias Ginter
Matthias Ginter (katikati)mlizi wa zamani wa Borussia Dortmund akitambulishwa na kocha wa Borussia Mgladbach na meneja wa timu hiyo.Picha: picture-alliance/Revierfoto

Marefa wa  Ujerumani wako tayari  kwa  ajili  ya  kutumia mfumo wa  video wa kuangalia  makosa  ya  refa  katika msimu  ujao na  hawata tumbukia  katika  utata na uchelewesho ulijitokeza  hivi  karibuni  katika  michezo  ya Confed Cup , amesema  mwamuzi  mmoja  Hellmut Krug leo. Krug  aliliambia  toleo la  gazeti  la  michezo  la Ujerumani Kicker  kwamba  marefa  wote wa  vodeo wamehusika  na  majaribio  kadhaa  ya  mtandaoni  na  nje ya  mtandao , na  pia  kama  marefa wanaoongoza mchezo.

Krug  ambaye  anaongoza  kitengo cha mradi wa  marefa wa  video (VAR) nchini  Ujerumani , amesema  uamuzi bila shaka  hautachukua muda  mrefu  kama  ilivyotokea katika kombe la  dunia  la  vijana  chini  ya  umri wa miaka  21 na kombe  la mabara Cofed Cup.

VAR itafanyiwa  majaribio  rasmi katika  msimu  huu  wa Bundesliga ,ambao shirikisho  la  soka  duniani  FIFA litaamua  Machi  mwakani  iwapo  mfumo huo utumike rasmi.

Videobeweis Confed Cup Kamerun - Chile
Maamuzi kwa vidio katika kandanda ni mfumo utakaotumika msimu huu katika BundesligaPicha: picture-alliance/dpa/FIFA.com

Na  katika  ligi  ya  England  Romelu Lukaku  ameiaga rasmi  FC Everton  wakati  akitafakari  maisha  yake  akiwa na  Manchester  United , baada  ya  kukamilisha  uhamisho wa  pauni  milioni 75, sawa  na  Euro milioni  85.5.

Pia  Klabu  ya  Premier  League  ya  England  ya Tottenham Hotspurs imesema  haiko  katika  mazungumzo ya  kununuliwa  baada  ya  kuzuka  taarifa  katika  vyombo vya  habari  vya  England kwamba  mnunuzi  ambaye anasaidiwa  na  mmiliki  wa  mtandao  wa  kijamii  wa Facebook  Mark Zuckerberg  anatafakari  kutoa  kiasi  cha pauni  bilioni  1, dola  bilioni 1.29  kuinunua  klabu  hiyo.

Belgien Nationalmannschaft Romelu Lukaku in Brüssel
Romelu Lukaku ambaye anahamia Manchester United msimu ujaoPicha: picture-alliance/dpa/Belga/V. Lefour

Gazeti  la  Sunday Times liliripoti jana  kwamba  kampuni ya  uwekezaji  ya  Marekani  Iconiq Capital  imefanya mazungumzo  na  kampuni  kadhaa  zinazotaka  kununua juu  ya  uwezekano  wa  kuinunua  klabu  hiyo.

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre / afpe /  ZR

Mhariri: Josephat Charo