1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano nchini Haiti

Hamidou, Oumilkher10 Aprili 2008

Wananchi wapiga kelele kulalamika dhidi ya ughali wa maisha

https://p.dw.com/p/DfR4
Mipira ya magari yatiwa moto na maduka kuvunjwa mjini Port-au-PrincePicha: picture-alliance/ dpa



Rais René Préval wa Haiti amewatolea mwito wananchi watulie ,baada ya waandamanaji kurejea upya majiani mjini Port-au Prince,klulalamika dhidi ya ughali wa maisha.


Akihutubia taifa kupitia Radio na televisheni ya nchi hiyo,rais René Préval amesema kwa kifaransa cha kienyeji:" "Poze",au Acheni ",akiwasihi wafanya fujo waache kutumia nguvu kwasababu anasema hazisaidii kuufumbua mzozo uliopo.


Rais Préval amezungumzia uwezekano wa kutolewa ruzuku ili kuimarisha kilimo cha bidhaa muhimu nchini humo.


Rais René Préval ametoa hotuba hiyo akiwa katika jengoi la bunge lililozungushwa senyenge na kulindwa vikali na vikosi vya kulinda amani vya umoja wa mataifa.


Kutoka eneo hilo mtu alikua akiona moshi uliotanda katika baadhi ya mitaa ambako waandamanaji wametia moto mipira ya magari wakiitaka serikali ipitishe hatua kukabiliana na kuzidi kuongezeka bei za bidhaa zote muhimu nchini humo.

 Kwa mfano bei ya mchele imepanda mara dufu katika kipindi cha miezi sita iliyopita.


Maduka yanavunjwa na baadhi ya barabara zimefungwa kwasababu ya machafuko.

"Hamkuona kitu bado,tunasubiri serikali ituambie inapangfa kupitisha hatua za aina gani,la sivyo mtatujua sisi ni nani."Amesema hayo Jeanti Mathieu,kijana wa miaka 21 aliyekua akisaidiana na wenzake kuweka vizuwizi majiani.


Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa Hedi Annabi anasema:


"Tunashuhudia maandamano makubwa dhidi ya serikali,yaliysosababishwa na kuzidi kuongezeka ughali wa maisha.Madhara ya usalama katika ghasia kama hizi yamedhihirika wiki iliyopita,tulipolazimika kuzihama ofisi zetu Les Cayes,kusini mwa nchi hii."


Wimbi la malalamiko limeanzia katika mji wa kusini wa Les Caye, jumatano iliyopita ambako watu wasiopungua watano waliuwawa kufuatia wiki nzima ya maandamano makali dhidi ya ughali wa maisha kataika nchi hiyo masikini kabisa miongoni mwa nchi za Amerika,ambako asili mia 80 ya wakaazi wake wanalipwa chini ya dala mbili kwa siku.


Jumanne iliyopita waandamanaji waliuvamia mji mkuu na kujaribu kulihujumu kasri la rais hjuku shughuli zote za mji mkuu zikipooza.Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa mataifa vilivyowekwa nchini humo tangu rais wa zamani Jean- Bertrand Aristide alaipoondolewa madarakani mwaka 2004 walilazimika kufyetua risasi za sandarusi na gesui za kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji.


Licha ya hali hiyo tete rais René Préval anasema serikali yake ambayo haina fedha,haiwezi kumudu kufuta ushuru wa bidhaa zinazoagiziwa kutoka nje.Amesema frédha hizo zinahitajiwa kwaajili ya ujenzi wa barabara na miradi mengine ya maendeleo.


Kabla ya hapo serikali ilitangaza vitega uchumi vya mamilioni ya dala katika sekta ya kilimo na miundo mbinu ili kukuza ajira na kuimarisha kilimo.


Lakini waandamanaji wanadai serikali ifutilie mbali  ushuru wa bidhaa muhimu za mahitaji ya kila siku ya raia kama kwa mfano mchele na maharagwe.


Rais Préval anasema muhimu ni kutoa ruzuku kwa bidhaa zinazolimwa nchiuni badala ya zile zinazoagiziwa kutoka nje.


►◄