1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano Thailand

15 Machi 2010

Vikosi vya jeshi nchini Thailand vimepelekwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bangkok, kuimarisha ulinzi, wakati ambao maelfu ya waandamanaji wanaoipinga serikali ya nchi hiyo, wakiwa wamekusanyika katika kambi za jeshi .

https://p.dw.com/p/MTOf
Waandamanaji mjini BangkokPicha: Holger Grafen

 Nia ni kushinikiza matakwa yao ya kuitisha uchaguzi.

Waandamanaji hao waliovalia fulana nyekundu na ambao wanamuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Thaksin Shinawatra, wameipa masharti serikali kulivunja bunge la nchi hiyo na kuitisha uchaguzi, ifikapo mchana wa leo. Ama sivyo kukabiliwa na maandamano makubwa, kama anavyoelezea zaidi kiongozi wao, Weng Tojirakarn,''Tunataka bunge livunje na uchaguzi mpya ufanywe. Lakini iwapo serikali itakataa kufanya hivyo, lazima iwajibike kwa lolote litakalotokea.''alisisitiza.

Hata hivyo, akiungwa mkono na jeshi la nchi hiyo, Waziri Mkuu wa Thailand, Abhisit Vejjajiva, ameyapinga masharti hayo yaliyotolewa na maelfu ya waandamanaji.

Akizungumza katika televisheni ya nchi hiyo, mapema leo asubuhi, amesema waandamanaji wamemtaka kulivunja bunge la nchi hiyo kabla ya mchana wa leo, lakini muungano wa vyama umekubaliana kuwa suala hilo halitawezekana.

Amesema uchaguzi ni lazima ufanyike kwa mujibu wa sheria zilizopo na kukiwa katika hali ya utulivu. Amesisitiza kuwa ni lazima pia wapate maoni ya watu wengine kuhusiana na mabadiliko hayo na si waandamanaji peke yao.

Thailand Militär
Wanajeshi wakipiga doria mjini Bangkok kwenye majengo ya serikaliPicha: AP

Wakati hali ikiwa tete, kikosi cha wanajeshi, polisi na askari wengine wa kulinda usalama kimetawanya katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bangkok, ambapo wanajeshi wapatao elfu 3 katika kambi ya jeshi ambako waziri mkuu wa nchi hiyo anaishi, wakiwasubiri wapinzani hao wawawasili katika eneo hilo.

Maandamano hayo, ambayo yalianza siku ya Ijumaa, mpaka jana yalikuwa yamefanyika kwa amani na utulivu huku yakiwakusanya watu takriban laki moja na elfu 50.

Wengi ya waandamanaji hao wamesafiri kutokea majimbo ya vijijini ya Thailand yaliyo masikini, kaskazini mwa nchi hiyo, wanamuunga mkono Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Thaksin Shinawatra, ambaye alipinduliwa katika mapinduzi ya mwaka 2006 na kwa sasa anaishi nje ya nchi hiyo, hususan Dubai, kutokana na kuogopa kufungwa gerezani kwa mashtaka ya rushwa.

No Flash Demo in Bangkok ###Achtung, nicht für CMS-Flash-Galerien###
Wafuasi wa Thaksin Shinawatra waliowasilikwa boti kutokea vijijini.Picha: AP

Katika hatua nyingine, licha ya kuongezeka hali ya wasiwasi kisiasa, fedha za kigeni zimekuwa zikimiminika  katika soko la hisa la Thailand kwa kufikia kiasi cha dola milioni 812 kwa zaidi ya kipindi cha wiki tatu zilizopita, ambapo wawekezaji wamekuwa wakitafuta faida kutoka katika eneo hilo linaloinukia kiuchumi la Kusini Mashariki mwa Asia, ambalo hali yake ya kiuchumi imekuwa ikirudi nyuma kwa haraka.

Wakati huohuo, wanajeshi wawili wamejeruhiwa kufuatia miripuko mitatu iliotokea katika kambi ya jeshi katikati mwa mji mkuu wa Bangkok.

Haijafahamika bado kama miripuko hiyo inahusiana na maandamano hayo.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp, Reuters)

Mhariri: Miraji Othman