1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron awahimiza washirika wa Ukraine wasiwe 'waoga'

Zainab Aziz
6 Machi 2024

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, amekariri kauli yake ya kupelekwa wanajeshi wa Ulaya nchini Ukraine na amewahimiza washirika wa Ukraine kutokuwa waoga katika kuiunga mkono nchi hiyo inapopambana na uvamizi wa Urusi.

https://p.dw.com/p/4dDLq
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akizungumza wakati wa Kongamano la Nyuklia kati ya Jamuhuri ya Czech na Ufaransa mjini Prague.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akizungumza wakati wa Kongamano la Nyuklia kati ya Jamuhuri ya Czech na Ufaransa mjini Prague.Picha: Michal Kamaryt/CTK/AP/picture alliance

Rais huyo wa Ufaransa EmmanuelMacron, amesisitiza kauli yake ya kutatanisha aliyoitoa wiki iliyopita kuhusu haja ya nchi za magharibi kuwapeleka wanajeshi wao nchini Ukraine. Kauli hiyo ilileta mshtuko kote barani Ulaya.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Gonzalo Fuentes/AFP/Getty Images

Rais wa Ufaransa amesema katika mkutano wa pamoja na mwenzake wa Jamuhuri ya Czech kwamba nchi hizo zinaungana katika kuiunga mkono Ukraine kwenye vita vyake na Urusi na kwamba ziko tayari kutafuta njia mpya za kuwasaidia Waukraine ili waweze kushinda vita hivyo.

Soma Pia:Zelensky: Dhamira ya kisiasa inahitajika kuisaidia Ukraine

Macron amesema, "Hakika tumefikia wakati katika historia ya Ulaya ambapo hatupaswi kuwa waoga. Naamini kuwa nchi zetu zote mbili zinafahamu kile kinachotokea. Ukweli ni kwamba vita vimeingia kwenye ardhi zetu na nguvu ambazo ni vigumu kuzuilika zinazidi kututishia kila siku kwa kutushambulia zaidi na zaidi."

Jamhuri ya Czech, inaupigia debe mpango wa kununua silaha kutoka nje ya bara la Ulaya kwa ajili ya Ukraine.

Hata hivyo msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa nchini Marekani John Kirby, amewaambia waandishi wa habari kwamba Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, hajawahi kutaka wanajeshi wa nchi za Magharibi wapelekwe kupambana na Urusi katika ardhi ya nchi yake bali amekuwa siku zote akiomba aongezewe zana za kivita ili aweze kupambana na uvamizi wa Urusi dhidi ya nchi yake ya Ukraine.

Soma Pia:Zelensky aomba msaada zaidi kutoka Magharibi

Vilevile washirika wengi wa Macron barani Ulaya walijibu kwamba hawatawapeleka wanajeshi wao huko nchini Ukraine mara baada ya Rais wa Ufaransa kutoa maoni yake hayo mnamo Februari 26.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius Picha: Maja Hitij/Getty Images

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistoriusalisema katika mkutano na waandishi na habari mjini Stockholm, baada ya kukutana na mwenzake wa Sweden Pal Jonson, kwamba kauli ya Macron haileti manufaa yoyote.

Mkuu wa kitengo cha ujasusi kinachoshughulikia ujasusi wa nje ya nchi nchini Urusi Sergei Naryshkin, amesema Rais wa Ufaransa kukataa kuondoa tamko lake la kuwapeleka wanajeshi wa Ulaya nchini Ukraine kupambana na askari wa Urusi ni jambo la hatari sana.

Vyanzo: AP/AFP/RTRE