1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron na Le Pen washambuliana katika mdahalo

Jane Nyingi
5 Aprili 2017

Zikiwa zimesalia siku 19 tu kabla ya kufanyika uchaguzi wa urais nchini Ufaransa, mwanasiasa  wa mrengo wa wastani, Emmanuel Macron, anaendelea kuonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kuibuka mshindi

https://p.dw.com/p/2akXg
Frankreich elf Präsidentschaftskandidaten treten in TV-Debatte gegeneinander an
Picha: picture alliance/abaca/J. Domine

Hapo jana wakati wa mdahalo wa urais ulioonyeshwa moja kwa moja kwa televisheni, wagombea wote 11 walitangaza sera zao za kisiasa, huku Macron akitoana kijasho na hasimu wake mkubwa Marine Le Pen hasa juu ya sera zake kuhusu bara Ulaya. 
Miongoni mwa maswala nyeti yaliyojadiliwa katika mdahalo huouliochukua karibu muda wa masaa manne, ni pamoja na kero zinazotokana na utandawazi, wasiwasi wa mashambulizi yanayofanywa na watu wenye misimamo mikali na pia hofu kuhusu hatma ya Umoja wa Ulaya. Wagombea wote 11 wa urais walishiriki, tisa wanaume na wawili wanawake.

Kwa mujibu wa kura za maoni, upinzani mkali katika uchaguzi huo wa tarehe 23 mwezi huu  ni kati ya mwanasiasa wa  mrengo wa kati Emmanuel Macron na kiongozi wa  chama  cha National Front, Marine Le Pen. Le Pen ataibuka katika raundi ya kwanza ya uchaguzi huo na kisha kupoteza kwa Macron katika marudio ya  uchaguzi huo tarehe 7 mwezi Mei. Walipoulizwa jinsi watakavyounda nafasi za ajira katika taifa ambalo idadi ya wasio kazi kwa miaka mingi imesalia kuwa asilimia 10, Macron alisema muhimu ni kuwa na soko huru, swala lilopingwa vikali na Le Pen. Macron pia aliahidi kupunguza kodi ya biashara, kulegeza sheria za kazi nchini Ufaransa na kuimarisha mazungumzo kati ya vyama  vya waajiri ili kusadia katika kujenga nafasi za ajira. “Kile ninachoahidi ni cha kweli, mabadiliko kamili ya kisiasa, mambo mapya, mbinu mpya kwasababu nina imani na taifa letu. Nina amani tunaweza kuyashinda matatizo ya kisasa yanayotokana na utandawazi ,na tunauwezo wa kufanya hilo." Alisema Macron.

Frankreich Wahlen - Macrons Wahlkampf
Mgombea wa urais Emmanuel MacronPicha: Getty Images/AFP/E. Feferberg

Macron alimshambulia Le Pen kutokana na sera zake hasa za  kutaka Ufanransa kujiondoa  kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, kusitisha utumizi wa sarafu ya Euro na kukabiliana na uhamiaji. Hata hivyo Le Pen alimjibu Macron na kumweleza hapaswi kujifanya ataleta mwamko mpya Ufaransa wakati ambapo ana fikra za kikale. Ni matamshi yaliyomgadhabisha Macron, na kusema “Samahani kukwambia hili, bi Le Pen,unachokisema hivi sasa ni uongo huo huo, tuliousikia  kutoka kwa baba yako miaka 40 iliyopita”. Maelezo hayo yalionekana kulenga juhudi za Le Pen za kukipa taswira mpya chama kilichoanzishwa na babake Jean Marie Le Pen, ili kuwavutia wapiga kura zaidi.
Baada ya kumalizika mdahalo huo mwanasiasa matata wa mrengo wa kushoto, Jean-Luc Melenchon  aliorodheshwa wa kwanza kama aliyetoa hoja zenye ushawishi, Le Pen akawa natika nafasi ya nne nyuma ya Macron na mgombea wa chama cha kisoshialisti  Francois Fillion. Asilimia 23 ya waliotazama mdahalo huo walisema kati ya wagombea wote 11 walirishishwa zaidi na sera za Macron na kisha mwanasiasa Melenchon, ambaye amendelea kupata umaarufu tangu mdahalo wa kwanza wa urais uliofanyika mwezi uliopita.

Frankreich Präsidentschaftskandidaten TV-Debatte - Marine Le Pen
Mgombe wa urais Marine Le PenPicha: Getty Images/AFP/L. Bonaventure

 

Mwandishi: Jane Nyingi/AP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef