1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron na Merkel wajadili uhamiaji mjini Marseille

Iddi Ssessanga
8 Septemba 2018

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wamekutana mjini Marseille, Ufaransa kukubaliana juu ya masuala kadhaa muhimu kuelekea mkutano wa kilele usiyo rasmi wa Umoja wa Ulaya Septemba 20.

https://p.dw.com/p/34WDX
Marseille Präsident Macron und Kanzerlin Merkel
Picha: Getty Images/AFP/C. Simon

Akimkaribisha kansela huyo wa Ujerumani katika kasri la Pharo katika mji wa Mediterrania wa Marseille, Macron alisema wangejadili "Changamoto kubwa ya siku, masuala kuhusu uhamiaji," pamoja na Brexit na kanda ya Euro, ambayo Macron anataka kuifanyia mageuzi makubwa.

Viongozi hao wawili wakuu wa Ulaya walikutana mjini Meseberg mwezi Juni ambako waliwasilisha bajeti mpya ya kanda ya Euro kama njia ya kuimarisha ushindani wa kiuchumi wa kanda hiyo.

Suala la Brexit limeendelea kuwa kipaumbele cha juu mnamo wakati Uingereza ikijiandaa kuondoka katika Umoja wa Ulaya ifikapo Machi 2019, ingawa ni machache tu yaliowekwa wazi kuhusu suala hilo na hadi sasa hakuna makubaliano kamili.

Marseille Präsident Macron und Kanzerlin Merkel
Rais Emmanuel Macron akimkaribisha kansela Angela Merkel katika kasri la Pharo mjini Marseille, Septemba 07.09.2018.Picha: picture-alliance/AP/C. Paris

Macron anategemea uungaji mkono wa Merkel kwa mapendekezo yake ya mageuzi ndani ya kanda ya sarafu ya Euro, ambayo yamekumbana na upinzani kutoka kwa mataifa mengine wanachama pamoja na baadhi ya wanasiasa wa Ujerumani.

Katika taarifa fupi baada ya mkutano huo, Merkel alisema "Ufaransa na Ujerumani zinao mkakati wa pamoja kuhusu uhamiaji.

"Tutafuatilia agenda ya Meseberg. Katika muda wa miezi michache ijayo, kutakuwa na uchaguzi wa Ulaya, lakini kati ya sasa na wakati huo, tunataka kukamilisha mambo kadhaa: Uendelezaji wa muungano wa sarafu, umoja wa kibenki na kuimarisha kanda ya sarafu ya euro. Hili linajumlisha pia mada kuhusu uhamiaji," alisema Merkel.

Viongozi hao wawili wanashinikiza kuwepo na mipango yenye ufanisi itakayoimarisha mipaka ya nje ya Umoja wa Ulaya, na wanataka kanda hiyo ionyesha mshikamano zaidi ili kupunguza shinikizo kwa mataifa wanakoingilia wahamiaji kama Ugiriki, Italia na Uhispania.

Ulaya inayojitegemea zaidi

Merkel alisema siku ya Ijumaa kuwa alikuwa na matarajio mazuri kwamba wanaweza kuendelea kuongoza njia kwenda mbele, kwa ajili ya Ulaya yenye kujitawala, na ambayo inaweza kutatua matatizo yake kwa uhuru.

FRANCE-GERMANY-DIPLOMACY
Rais Macron akishikana mikono na kansela Merkel kabla ya mkutano wao.Picha: Getty Images/AFP/C. Simon

Viongozi hao walikubaliana mwezi Juni kuhusu mapendekezo ya kuanzisha bajeti ya kanda ya euro kuanzia mwaka 2021 ndani ya mfumo wa sasa wa kifedha, pamoja na kanuni sawa za kibenki na mfumo wa uokozi wa benki za ukopeshaji zinazofeli.

Macron na Merkel walitarajiwa pia kujadili azma ya mbunge wa Ujerumani Manfred Weber kuwania nafasi ya Rais wa Halmahsuri Kuu ya Umoja wa Ulaya mwaka 2019. Weber ni mwanachama wa muungano wa vyama vya kihafidhina wa Merkel.

Ingawa Merkel anaunga mkono ugombea wa Weber, rais wa Ufaransa hana uwezekano mkubwa wa kumuidhinsha mgombea kutoka kambi ya vyama vya mrengo wa kati-kulia wa European People's Party EPP, ambao unahusisha pia chama waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban cha Fidesz.

Msemaji wa Merkel Steffen Seibert alisema kabla ya kuondoka kwa kansela huyo siku ya Ijumaa kuwa viongozi hao wawili pia wangezungumzia msimamo wao wa sera ya kigeni kuhusu Syria, Ukrain na Balkan magharibi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpa, afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman