1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Madaktari wasio na mipaka wahofia wakimbizi kukosa misaada

Sudi Mnette
13 Juni 2023

Shirika la Madaktari wasio na mipaka (MSF) limesema maelfu ya wakimbizi wa Sudan waliokimbilia nchini Chad kukwepa mapigano wako hatarini kukosa misaada ya kiutu na tiba katika kipindi hiki cha karibu na mvua.

https://p.dw.com/p/4SVF7
Wakimbizi wa Sudan wakiwa wamekaa katika kambi ya Borota iliyoko katika mpaka wa Chad na jimbo la Darfur, Sudan.
Mzozo wa kimamlaka nchini Suda umesababisha raia wengi kuyakimbia makazi yao na kwenda mataifa ya jirani.Picha: Blaise Dariustone/DW

Kiongozi wa mpango wa huduma wa MSF kwa Chad, Audrey van der Schoot amesema mafuriko ambayo kwa kawaida hutokea katika kipindi hiki cha mwaka yanaweza kuwatenga wakimbizi na jamii zinazowahifadhi katika eneo la Sila huko mashariki mwa Chad na maeneo mengine yanayopakana na Sudan.

Ameongeza kwa kusema mvua hiyo pia italeta hatari kubwa ya magonjwa yanayoenezwa na maji na ya kuambukiza kutokana na upatikanaji duni wa maji safi na usafi wa mazingira.

Zaidi ya Wasudan 100,000 wameingia Chad tangu mzozo ulipozuka nchini Sudan mwezi Aprili, na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR lilionya kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka mara mbili katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.