1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana Chemnitz kupinga au kuunga mkono uhamiaji

Caro Robi
2 Septemba 2018

Maelfu ya watu waliandamana Jumamosi(01.09.2018) mjini Chemnitz baada ya wimbi la vurugu zilizochochewa na ubaguzi wa rangi kufuatia mwanamume Mjerumani kuuawa kwa kudungwa kisu na wanaodaiwa kuwa wahamiaji.

https://p.dw.com/p/34Aaj
Deutschland AfD-Kundgebung und Gegenproteste in Chemnitz ziehen tausende Demonstranten an
Picha: Getty Images/S. Gallup

Polisi imesema maandamano ya Jumamosi yaliyowavutia takriban watu 8,000, yalikamilika kwa amani licha ya kuwepo hali ya taharuki katika mji huo wa Chemnitz hasa jioni. Waandamanaji wanaounga mkono makundi na vyama vya kisiasa vya mrengo wa kulia walibeba mabango yaliyokuwa na picha za waathiriwa wanaodaiwa kushambuliwa na wahamiaji.

Kuwa na moyo badala ya chuki

Baadhi ya waandamanaji hao waliimba Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anapaswa kuondoka madarakani huku wakipeperusha bendera za Ujerumani. Kwa upande mwingine, waandamanaji wanaoiunga mkono serikali na kuyapinga makundi yenye misimamo mikali dhidi ya wageni walibeba mabango yaliyoandika ujumbe wa kuwa na moyo wa imani badala ya chuki.

Chemnitz Kundgebung des Bündnisses Chemnitz Nazifrei unter dem Motto «Herz statt Hetze»
Bango linalosema kuwa na moyo badala ya chukiPicha: picture alliance/dpa/M. Skolimowska

Idadi kubwa ya polisi ilishuhudiwa katika maandamano hayo baada ya wiki iliyopita, maafisa hao wa usalama kuzidiwa nguvu na maelfu ya wafuasi wa makundi yenye misimamo mikali. Hayo yote yametokana na mauaji ya raia wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 35 aliyedungwa kisu. Watu wawili, mmoja raia wa Iraq na Msyria wamekamatwa kwa kudaiwa kuhusika na mauaji hayo.

Kufuataia kukamatwa kwa wahsukiwa hao, magenge ya watu yalianza kuwashambulia watu walioonekana kuwa na asili ya kigeni mitaani katika mji huo wa Chemnitz.

Uhamiaji suala moto Ujerumani

Miongoni mwa wageni walioshambuliwa ni kutoka Afghanistan, Syria na Bulgaria. Kulingana na makadirio ya polisi, maandamano ya Jumamosi yaliwavutia wafuasi 4,500 wa makundi mbalimbali wa mrengo wa mrengo wa kulia ikiwemo wafuasi wa chama cha kisiasa kinachowapinga wageni Ujerumani Alternative für Deutschland AfD na vuguvu linalowapinga Waislamu Ujerumani PEGIDA.

Waandamanaji wengine 3,500 wanaounga mkono sera ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ya kuwapokea wahamiaji pia waliandamana Chemnitz.

Deutschland | Rechte Demo in Chemnitz
Maelfu ya waandamanaji mjini Chemnitz waliobeba bendera ya UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/R. Hirschberger

Shambulizi hilo la Chemnitz na wimbi la maandamano kwa mara nyingine limezua mjadala mkali kuhusu uamuzi wa mwaka 2015 wa serikali ya Merkel kuwapokea maelfu kwa maelfu ya wahamiaji nchini Ujerumani, suala ambalo limekuwa changamoto kubwa kisiasa kwa Kansela huyo, hasa katika eneo la mashariki mwa Ujerumani ambako ni ngome ya chama cha AfD.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas aliandika katika ukarasa wa Twitter kuwa vita vya pili vikuu vilianza miaka 79 iliyopita, ambapo Ujerumani ilisababisha machungu makubwa Ulaya na iwapo kwa mara nyingine, watu hivi sasa wanaandamana mitaaani wakipiga saluti ya Wanazi, basi kutokana na historia ya zamani ya Ujerumani, hawatakuwa na budi bali kuilinda kwa nguvu zote demokrasia.

Maas ameongeza kusema hawataruhusu wafuasi wa mrengo wa kulia wenye misimamo mikali kuiharibu nchi yao na demokrasia, sio Chemnitz, Saxony wala kokote Ujerumani.

Mwandishi: Caro Robi

Mhariri: Isaac Gamba