1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSerbia

Maelfu waandamana tena Serbia kupinga matokeo ya uchaguzi

26 Desemba 2023

Maelfu ya wafuasi wa upinzani nchini Serbia walikwenda hadi kituo cha polisi cha mji mkuu, Belgrade kuonesha mshikamano na wale waliokamatwa wakati wa vurumai iliyozuka siku moja iliyopita kupinga matokeo ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/4aZi7
Vuramai nchini Serbia
Vurumai nchini Serbia Picha: Filip Stevanovic/AA/picture alliance

Mkusanyiko huo jana ulikuwa ni wa siku ya 8 mfululizo wa maandamano ya upinzani ambayo kwa sehemu kubwa yamekuwa ya utulivu lakini yaligeuka kuwa mapambano makali usiku wa Jumapili.

Wafuasi wa upinzani walifanya vurugu wakiyapinga matokeo ya uchaguzi wa bunge na serikali za mitaa yaliyokipa ushindi mkubwa chama cha rais Aleksandar Vucic cha Serbian Progressive, SNS. Wanasema ushindi wa chama hicho umetokana na wizi wa kura na udanganyifu wakati wa uchaguzi uliofanyika Disemba 17.

Rais Vucic mwenyewe amelaani wimbi hilo la maandamano ambalo amesema limechochewa na njama za mataifa ya kigeni.