1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu waandamana Yemen

3 Februari 2011

Zaidi ya Wayemeni 20,000 wamemiminika katika barabara mbalimbali za mji wa Sana'a hii leo, wakitaka mabadiliko katika serikali ya rais Ali Abdullah Saleh.

https://p.dw.com/p/109lP
'Siku ya Hasira' Yemen.Picha: picture alliance/dpa

Katika siku walioiita 'siku ya hasira', waandamanaji nchini Yemen wanasema pendekezo la rais Ali Abdullah Saleh la kujiuzulu ifikapo mwaka 2013 halitoshi.

Ali Abdullah Salih
Rais Ali Abdullah Saleh wa Yemen.Picha: picture-alliance/ dpa

Maandamano zaidi dhidi ya serikali yalitarajiwa kufanyika nchini Yemen ambapo rais Ali Abdullah Saleh amekuwa akitawala kwa zaidi ya miongo mitatu na wafuasi wa kiongozi huyo walionekana wakizunguka katika mji mkuu wakiwaomba wananchi kwa kutumia vipaza sauti, kujiunga na maandamano ya kuiunga mkono serikali.

Lakini kufikia leo alfajiri, waandamanaji wanaoipinga serikali walifanikiwa kukusanya umati mkubwa, tangu msururu wa maandamano kulikabili taifa hilo la Kiarabu wiki mbili zilizopita, na yalioyoshawishiwa na maandamano yaliomuondoa madarakani kiongozi wa Tunisia na kumtishia pia rais wa Misri.

Nje ya chuo kikuu cha Sana'a waandamanaji walipiga kelele wakisema kuwa wananchi wanataka mabadiliko, na kuwa wanapinga ufisadi na udikteta.

Utawala wa rais Saleh

Rais Saleh ambaye ameona vurugu linalozagaa katika mataifa ya Kiarabu aliashiria hapo jana kuwa ataondoka madarakani, awamu yake itakapomalizika mwaka 2013, na miongoni mwa ahadi nyingine alizotoa alisema kuwa mwanawe wa kiume hatorithi uongozi wa serikali hiyo.

Hatua hii ya kutetereka kwake wazi, imenuiwa kuepusha mzozo katika nchi ya Yemen iliyo mshirika mkuu wa Marekani na iliyo dhidi ya kundi la kigaidi la Al Qaeda, na ni jitihada za kiongozi huyo kuepuka makabiliano na upinzani ambayo huenda yakahatarisha kuzusha mapinduzi katika taifa hilo maskini, yalio mfano wa Misri.

Proteste im Jemen
Picha: picture alliance / landov

Mwandalizi wa maandamano ya leo nchini humo, Wael Mansour, amesema wananchi wa Yemen hawajaridhishwa na pendekezo la rais Saleh, na kuwa maandamano ya leo yanatarajiwa kutoa shinikizo zaidi na jipya kwa rais Saleh atakayelazimika kutoa mapendekezo zaidi kwa upinzani. Wael aliyasema haya pasi kufafanuwa mapendekezo hayo ni yapi.

Majukumu ya Yemen

Hatari ni kubwa kwa Yemen iliyokaribu kutangazwa kuwa taifa lililoshindwa , wakati likijaribu kupigana dhidi ya kuzuka upya kwa tawi la kundi la kigaidi la Al Qaeda, kutuliza kujitenga kwa sehemu ya kusini, na kushinikiza amani miongoni mwa waasi wa kishia kaskazini ya nchi hiyo, yote haya ikiwa ni katika jitihada za kuutokomeza umaskini. Thuluthi moja ya wananchi wa Yemen wanakabiliwa na njaa kubwa.

Marekani inamtegemea sana rais Saleh kusaidia kupambana na tawi la kundi la Al Qaeda nchini humo, ambalo limeilenga pia nchi jirani ya Saudi Arabia ambayo ni mtoaji mkubwa a mafuta duniani.

Jemen Demonstration
Picha: DW

Kutoimarika kwa Yemen huenda kukazuwa hatari kubwa ya kisiasa na kiusalama kwa mataifa ya Ghuba.

Shirika la kitaifa la habari nchini Yemen, Saba, limemnukuu rais wa Marekani Barack Obama katika mawasiliano ya simu na rais Saleh kuwa anamuunga mkono katika mpango wake.

Mwandishi: Maryam Abdalla/Rtre
Mhariri:Othman Miraji