1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Maafisa wa zamani wa ujasusi washiriki katika vita Sudan

Tatu Karema
28 Juni 2023

Maelfu ya maafisa wa zamani wa ujasusi chini ya utawala wa rais wa zamani wa Sudan Omar al- Bashir wanadaiwa kupigana pamoja na jeshi la Sudan katika vita nchini humo. Vyanzo vinne vimearifu.

https://p.dw.com/p/4TB2P
Sudan | Waffenstillstand General Abdel Fattah al-Burhan
Picha: Sudanese Armed Forces/REUTERS

Kwa muda mrefu, jeshi la Sudan limekanusha shtuma za wapinzani wake katika kikosi cha wanamgambo wa RSF nchini humo kwamba linategemea wafuasi wa Bashir wanaolaumiwa kwa ukatili.

Akijibu swali kutoka shirika la habari la Reuters, afisa mmoja wa jeshi alisema kuwa jeshi la Sudan halina uhusiano wowote na chama cha siasa ama itikadi na kuongezea kuwa ni taasisi ya kitaaluma.

Akizungumza kwa sharti la kutotambulishwa, afisa mmoja wa jeshi anayefahamu shughuli za kijeshi, amesema takriban wanachama elfu 6 wa idara ya ujasusi walijiunga na jeshi hilo wiki kadhaa kabla kuanza kwa mapigano na kwamba wanapigana kuiokoa nchi hiyo.

Maafisa wa zamani wa idara ya kitaifa ya ujasusi na huduma za usalama iliyovunjwa, wamethibitisha takwimu hizo.

Vita nchini Sudan vyaibua kumbukumbu ya mauaji katika eneo la Darfur

Vita nchini Sudan vimeibua kumbukumbu mbaya katika eneo linalokumbwa na mzozo la Darfur ambapo makundi ya kujihami yanashtumiwa kwa kuwalenga raia kwa misingi ya kikabila na kuzua hofu ya mauaji mapya ya halaiki.

Inaam kama wengine waliohojiwa na shirika la Habari la AFP, hakutumia jina lake rasmi kwa hofu ya mashambulizi dhidi ya jamii yake, ni mtetezi  wa haki za binadamu na manusura wa ghasia hizo za Darfur.

Inaam anasema alitoroka eneo hilo hadi nchi Jirani ya Chad na kuongeza kuwa washambuliaji waliteketeza kila nyumba katika eneo hilo na kumuuwa kakake mbele yake.

Mashirika ya misaada yasema mapigano hayo yamezidisha mzozo wa muda mrefu wa kibinadamu

Mohammed Hamdan Dagalo
Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo - Kiongozi wa RSFPicha: AP/picture alliance

Ushuhuda kama huo, umezua wasiwasi kuhusu kurudiwa kwa historia ya umwagaji damu katika eneo la Darfur, ambapo mnamo mwaka 2003, Bashir, aliawatuma wanamgambo wa kikabila wa kiarabu katika kampeini kali kukomesha uasi usiokuwa wa waarabu dhidi ya kile kilichoonekana kuwa ukosefu wa usawa.

Mashirika ya misaada yanasema kuwa mapigano hayo yamezidisha mzozo wa muda mrefu wa kibinadamu, baada ya kuvamiwa kwa kliniki, na maghala ya chakula kuharibiwa huko Darfur.

Shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka MSF, limeliambia shirika la Habari la AFP kwamba mapigano hayo hayajatishia tu maisha kupitia vita vya moja kwa moja lakini pia kuzuia upatikanaji wa huduma za matibabu.

Mkimbizi mwingine , mwalimu Ibrahim Issa, ameiambia AFP alifanikiwa kutoroka kile alichokiita jehanam katika eneo la El Geneina ambapo mapigano yaliibua kumbukumbu ya miaka ya 2003 na 2004 ambapo mtu aliuawa kwasababu ya kabila lake.

Maafisa wa matibabu wa shirika la MSF nchini Chad, wameripoti kuwatibu wakimbizi waliokuwa na majeraha ya risasi waliokuwa wamelengwa walipokuwa wakijaribu kutoroka mji huo.