1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya wakimbizi wawasili Austria na Ujerumani

1 Septemba 2015

Wakimbizi hao wameingia nchini Austria na Ujerumani baada ya Hungary kuruhusu treni kupita katika mji mkuu wake. Hii ni hatua iliyowashtua maafisa wa serikali za Austria na Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1GOss
Wakimbizi wakiwa katika kituo cha treni cha kimataifa mjini Budapest.
Wakimbizi wakiwa katika kituo cha treni cha kimataifa mjini Budapest.Picha: Reuters/L. Balogh

Kwa mujibu wa msemaji wa polisi ya Austria, jumla ya wahamiaji 3,650 waliwasili nchini humo siku ya Jumatatu, ikiwa ndiyo idadi kubwa zaidi ya wakimbizi kuwasili ndani ya siku moja mwaka huu.

Wakati maelfu ya wanaume, wanawake na watoto wanaokimbia vita Syria wakiendelea kuwasili kutokea Ulaya mashariki, maafisa waliozidiwa na wingi wao walibaki tu kutazama huku mamia ya wahamiaji, wengi wao bila viza, wakishuka katika kituo cha treni cha Vienna Magharibi, ili kupanda treni za kuendelea na safari yao hadi Ujerumani, ambayo ndiyo nchi inayopendelewa na wengi.

Maafisa mjini Budapest waliwaruhusu wahamiaji waliokuwa wamekwama kwa siku kadhaa katika makambi ya muda kupanda treni kwenda maeneo yao ya mwisho kaskazini mwa Ulaya.

Serikali ya Hungary imeikosoa Ujerumani kwa kulegeza sheria za ukimbizi, hatua iliyolenga kuyapunguzia shinikizo mataifa ya kusini ambako wakimbizi wanafikia kwa kutumia usafiri wa bahari, ikisema hatua hiyo inajenga tu matumaini ya wahamiaji haramu.

Shirika la habari la Hungary limesema kituo kikuu cha kimataifa cha usafiri wa treni kimefungwa mjini Budapest, huku mamia ya wakimbizi wakisubiri. Msemaji wa serikali ya Hungary ameeleza hatua ya kufungwa kwa kituo hicho ni utekelezaji wa sheria ya Umoja wa Ulaya kulingana na matamshi yaliyotolewa na kansela Angela Merkel siku ya Jumatatu.

Wakimbizi wakiwasili katika kituo cha treni ya Vienna nchini Austria.
Wakimbizi wakiwasili katika kituo cha treni ya Vienna nchini Austria.Picha: Reuters/L. Foeger

Mgogoro kwa Umoja wa Ulaya

Mtiririko huo wa wakimbizi umegeuka kuwa mgogoro kwa Umoja wa Ulaya, ambao uliondoa vizuizi vya mpakani kati ya mataifa 26 ya eneo la Schengen, lakini sheria zake zinawataka wanaotafuta hifadhi kufanyia maombi katika nchi ya kwanza ya Umoja wa Ulaya wanakofikia, jambo ambalo limekuwa likipuuzwa kwa muda mrefu.

Kwa kuzingatia sheria za Umoja wa Ulaya, msemaji wa polisi ya Austria, Patrick Maierhofer, alisema wale tu waliokuwa hawajaomba hifadhi nchini Hungary ndiyo wangeruhusiwa kuingia, lakini walizidiwa na idadi kubwa na treni hizo ziliachwa kuendelea na safari zake. Maierhofer amesema kuwa bado wanaendela na mchakato wa kuhakiki ni wangapi hasa kati ya wahamiaji hao ni waombaji wa hifadhi.

Katika kuwaunga mkono wahamiaji, watu 20,000 waliingia mitaani mjini Vienna Jumatatu jioni kupinga kunyanyaswa kwa wakimbizi hao, huku maafisa wandamizi serikalini wakihudhuria ibada ya misa ya wakimbizi 71 waliyokutwa wamekufa katika lori wiki iliyopita.

"Hatuwezi kutatua matatizo yote lakini tunapaswa kuwa tayari kupokea ushauri na kuwa na moyo mkunjufu," alisema Willi Resetarits, mwanamuzi na mwanaharakti wa haki za binaadamu aliyeshiriki maandamano hayo.

Mgogoro wa wakimbizi unaozidi kupamba moto umeigawa jumuiya wa Ulaya yenye mataifa wanachama 28 kuelekea mkutano wa dharura Septemba 14, ambapo viongozi wa mataifa ya Ulaya Magharibi wakitoa wito wa kufongeza juhudi za kuwaisaidia wahamiaji wanaowasili, huku mataifa yaliyoko kwenye mipaka ya mashariki mwa Ulaya yakipambana kumudu hali hiyo.

Wakiwasili katika kituo kikuu cha treni mjini Munich Ujerumani.
Wakiwasili katika kituo kikuu cha treni mjini Munich Ujerumani.Picha: Reuters/M. Dalder

Merkel akosoa msimamo wa Slovakia

Akizungumza wiki mbili kabla ya duru hiyo ya mazungumzo kuhusu mgogoro huo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ameonya juu ya kuharibi kile alichokitaja kuwa ni uhusiano wa karibu wa Ulaya na haki za kimataifa za kiraia katika kushughulikia wakimbizi.

Akizikosoa bila kuzitaja bayana nchi kama Slovakia, zilizosema zitawakataa wakimbizi kutoka mataifa ya Waislamu wengi, Merkel alisema, "Tukianza kusema hatuwataki Waislamu, hilo halitakuwa jambo zuri na linakwenda kinyume na moyo wa Ulaya na hatuwezi kuliruhusu."

Kwa upande wake Austria imeto wito wa kuondoa ufadhili wa Umoja wa Ulaya kwa mataifa yanayokataa kuchukuwa sehemu yao ya wakimbizi, na waziri mkuu wa Poland Ewa Kopacz alisema nchi yake nuhenda ikaongoeza idadi ya wakimbizi iliyokuwa tayari kuchukuwa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre,ape,dpae

Mhariri: Mohammed Khelef