1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya wanafunzi waandamana duniani dhidi ya tabia nchi

John Juma
24 Mei 2019

Waandaaji wa maandamano ya wanafunzi wameitisha maandamano katika zaidi ya miji 10 duniani. Maelfu kwa maelfu ya wanafunzi wanaandamana kushinikiza viongozi wa dunia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/3J0Uz
Fridays for Future Demo Klimawandel Demonstration
Picha: picture-alliance/dpa/D. Crosling

Maelfu kwa maelfu ya wanafunzi ulimwenguni kote leo wanaandamana katika miji mbalimbali katika kile kinaitwa siku ya kimataifa ya maandamano ya wanafunzi. Maandamano hayo yanalenga kushinikiza viongozi wa dunia kuchukua hatua muafaka za kukabiliana athari za mabadiliko ya tabia nchi. 

Madarasa katika miji mingi mikuu duniani yamebaki matupu bila wanafunzi, baada ya waandalizi wa maandamano ya wanafunzi maarufu kama 'Fridays for Future', kuitisha maandamano katika zaidi ya nchi 100 leo.

Wanafunzi wamejitokeza katika miji kadhaa barani Ulaya, kaskazini mwa Amerika na Asia huku wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe kama vile: "Hakuna Sayari nyingine", "Mnauharibu mustakabali wetu", "Maisha yetu ya kesho yako mikononi mwenu", na "Mmsiwe Trump", miongoni mwa mengine kadhaa.

Licha ya miongo mitatu ya maonyo, kumezidi kuwa na ongezeko la gesi zinazochafua hewa na kuzidisha viwango vya joto ulimwenguni. Mwaka 2017 na hata mwaka jana ongezeko la gesi ukaa lilipindukia kupita viwango vya awali.

Baadhi ya wanaharakati wanaotaka hatua zichukuliwe kukabili athari za mabadiliko ya tabia nchi wakiandamana Brooklyn Bridge Marekani.
Baadhi ya wanaharakati wanaotaka hatua zichukuliwe kukabili athari za mabadiliko ya tabia nchi wakiandamana Brooklyn Bridge Marekani.Picha: Reuters/B. McDermid

Onyo la wanasayansi

Wanasayansi wanasema kuwa kuendelea kuruhusu gesi ukaa hewani katika viwango vyake vya sasa kutaifanya dunia kuwa sayari ambayo binadamu hawezi kuishi.

Waandamanaji wanasikitishwa na viongozi wa dunia kutochukua hatua muafaka. Jose Ferreras mwenye umri wa miaka 22 na ambaye ni mwanafunzi kutoka Uhispania anayeshiriki maandamano hayo amesema:

"Tunaamini kumekuwa na ukosefu wa uwajibikaji kutoka kwa wanasiasa katika miaka iliyopita, tangu suala la mabadiliko ya tabia nchi lianze kujadiliwa miaka 27 iliyopita. Kwa hivyo tunawataka wajitolee kuchukua hatua madhubuti dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi."

Juhudi za mwanafunzi mwanaharakati Greta Thunberg

Greta Thunberg amekuwa akiongoza maandamano ya wanafunzi kuwashinikiza viongozi wa dunia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Greta Thunberg amekuwa akiongoza maandamano ya wanafunzi kuwashinikiza viongozi wa dunia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.Picha: picture-alliance/V. Jones

Msichana mwanaharakati kutoka Sweden mwenye umri wa miaka 16, Greta Thunberg, ambaye amekuwa akiongoza maandamano hayo ameonya kuwa muda unayoyoma na hatua sharti zichukuliwe.

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, Thunberg ambaye ameshateuliwa kushindania tuzo la amani la Nobel, kutokana na juhudi zake za uanaharakati amekadiria kuwa zaidi ya wanafunzi 10,000 wamejitokeza kuandamana mjini Stockholm.

Hapa Ujerumani, waandaaji wa maandamano hayo wamekadiria kuwa zaidi ya wanafunzi 300,000 wamejitokeza.

Wakati wanafunzi wakiandamana kote duniani, wawakilishi wa mataifa yanayokutana katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira nchini Kenya wametangaza kuwa wamekubaliana kupunguza zaidi mifuko ya plastiki katika mwongo ujao.

Hata hivyo, wataalamu wameonya kuwa ahadi zinazolenga tu kukabiliana na ongezeko la joto duniani kutokana na matendo ya wanaadamu haitatosha ikiwa uchafuzi wa hewa kutokana na gesi za viwanda hautakabiliwa kikamilifu.

Vyanzo: AFPE