1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko ya Pakistan yaitia wasiwasi Marekani

Josephat Nyiro Charo9 Agosti 2010

Marekani inatiwa wasiwasi na hatma ya kampeni yake ya kupambana na makundi ya wapiganaji walioko kwenye maeneo ya mipaka ya Afghanistan na Pakistan

https://p.dw.com/p/OfcY
Mama akiwabeba watoto wake huko Muzaffargarh, PakistanPicha: AP

Wanajeshi wa Pakistan wamelazimika kuziacha harakati za kupambana na wanamgambo na kushughulika katika operesheni ya uokozi kwa sababu ya mafuriko yaliyoigubika nchi hiyo. Mimea na mifugo vimeharibiwa na mafuriko hayo ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu alfu moja na wengine zaidi ya milioni 10 kuachwa bila makaazi. Hali hiyo inaaminika kuwa itaiwia vigumu bajeti ya serikali ya Pakistan.

Marekani inatiwa wasiwasi na hali hiyo ya Pakistan hasa ukizingatia kuwa mipango yake ya kuanzisha miradi ya maendeleo nchini humo huenda ikasusua. Hii ni kwa sababu juhudi zote kwa sasa zinaelekezwa kuwasaidia wahanga wa mafuriko walioachwa bila makazi wala njia za kuyakimu mahitaji yao ya kila siku. Wanajeshi wa Pakistan wamelazimika pia kuingia katika mkumbo huo jambo linaloihatarisha hali ya usalama hususan kwenye maeneo ya mpakani na Afghanistan ambako wapiganaji wa Taleban wanaendesha harakati zao.

Kwa mujibu wa mchambuzi wa masuala ya Pakistan wa taasisi ya Maendeleo ya Marekani, Brian Katulis, janga hilo litaitatiza bajeti ya serikali ya Pakistan inayofanya kila iwezalo kuwasaidaia watu wake walioathiriwa na mafuriko. Kauli hizo zinaungwa mkono na Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayehusika na janga hilo Jean-Maurice Ripert.

Mwaka 2001 Pakistan ilijiunga na operesheni ya kupambana na uasi inayoongozwa na Marekani, ambayo mpaka sasa imegharimu kiasi cha zaidi ya dola bilioni 35 katika kipindi cha miaka minane iliyopita. Gharama hizo zimeuathiri uchumi wa Pakistan ambayo inakabiliwa pia na matatizo ya umeme usioaminika, mfumko wa bei za bidhaa na idadi ndogo ya wawekezaji.

Itakumbukwa kuwa mwezi wa Novemba mwaka 2008,Pakistan ililazimika kuligeukia Shirika la Fedha Duniani,IMF, ili kupata mkopo wa dola bilioni 10.66 utakaotumika kuyalipa madeni yake ya kitaifa. Mpaka sasa bado inajitahidi kuvitimiza vigezo vya mkopo huo wa dharura. Kwa upande wake, serikali ya Marekani ina mipango yake ya maendeleo mahsusi kwa Pakistan itakayogharimu kiasi cha dola bilioni 7.5 katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Miradi hiyo ni ya maendeleo. Ili kulifanikisha hilo, Wizara ya Mambo ya Nje imekuwa ikishauriana na serikali ya Pakistan kuhusu miradi itakayoanzishwa ambayo inajikita katika masuala ya kuimarisha huduma za maji na nishati pamoja na kilimo ambacho ndio uti wa mgongo wa uchumi wake.

Kiasi kidogo cha fedha hizo huenda zikatumiwa kupambana na janga la mafuriko yanayoendelea kusababisha athari na maafa. Hata hivyo, Marekani itashirikiana na wafadhili wengine ili kuisadia Pakistan inayolazimika kutoa tathmini kamili ya msaada unaohitajika. Akizungumza na Shirika la habari la Reuters, Rajiv Shah anayelisimamia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani,USAID, alisema kuwa bila shaka wanaweza kuipangua mipango yote ya matumizi ya fedha ila kukabiliana na tatizo hilo ila majanga yanasababisha miradi ya maendeleo kusuasua.

Wakati yote hayo yakiendelea maafisa wa serikali ya Marekani wamelazimika kutolijadili suala hilo hadharani ukizingatia kuwa serikali ya Pakistan imeshindwa kukabiliana na janga lenyewe. Jambo jengine linaloitatiza hali yote, Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan alianza ziara rasmi ya mataifa ya UIaya pindi gharika lilipoanza. Kwa sababu ya hali hiyo, mashirika ya msaada yaliyo na mafungamano na makundi ya wapiganaji yametumia mwanya huo kusambaza misaada jambo linalowaimarisha kwa kuibadili mitazamo ya wakazi wa eneo hilo.

Kulingana na Bruce Riedel wa taasisi ya Brookings, serikali ya Pakistan inajitahidi kukabiliana na janga hilo ila makundi ya wapiganaji wa Kiislamu tayari wapo katika eneo la tukio na wanasambaza misaada ya kila aina. Kundi kubwa zaidi linalohusika na harakati hizo ni Jamaat-ud-Dawa linaloaminika kuwa na mafungamano na kundi la wapiganaji la Lashkar-e-Taiba linalonyoshewa kidole kuwa lilihusika katika mashambulio ya mabomu ya Mumbai ya mwaka 2008. Hata hivyo, Shirika la Marekani la USAID limezikanusha kauli hizo hasa baada ya shambulio la kujitoa muhanga lililotokea kwenye eneo la Peshawar lililo kaskazini mwa Pakistan.

Kwa upande wake, Marekani inataraji kuwa harakati zake za kuisaidia Pakistan kupambana na athari za mafuriko hayo zitafanikiwa kuubadili mtazamo wa serikali wa raia wa nchi hiyo.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya-RTRE

Mhariri: Josephat Charo