1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini: Theresa May anusurika kura ya kutokuwa na imani

Sekione Kitojo
13 Desemba 2018

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha zaidi hii leo(13.12.2018) na suala la kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu wa Uingereza  Theresa May, mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mazingira nchini Poland.

https://p.dw.com/p/3A0yi
Theresa May
Picha: picture-alliance/empics

Mhariri  wa  gazeti  la Fuldaer Zeitung  likiandika kuhusiana  na  kura  hiyo  ya  kutokuwa  na  imani  na  waziri  mkuu Theresa  May  anaandika:

Uingereza  na  Ulaya  zinaweza  sasa  kushusha  pumzi. Kwa mtafaruku  wote  uliotokea   katika  siasa  za  ndani  nchini Uingereza mwanamke  kiongozi  Theresa  May  bado  anaendelea kubakia  katika  ofisi  ya  waziri  mkuu  katika  mtaa  wa  Downing namba  10. Katika  kikundi cha  wabunge  wa  chama  cha Conservative ambao  hawapendelea  njia  anayochukua  May  katika suala  la  Brexit, hofu  ilikuwa  kubwa, kwamba  nchi  hiyo  katika wakti  huu  mgumu  inaweza  kutumbukia  katika  hali  ya  kukosa kiongozi. Wingi  uliowezesha  May  kushinda  kutoka  katika  kundi lake ni wa  kutia  moyo. Haikupatikana  theluthi  mbili  ya  wabunge ambao  hawataki abakie  katika  madaraka. Wakati  mwingine matokeo  kama  hayo  yanaweza kumlazimisha  waziri  mkuu kujiuzulu. Lakini  huu  si  wakati  wa  kawaida  mjini  London. Kizungumkuti  kwa  May, kwamba  bungeni  hana  wingi  kwa  ajili  ya mkataba  na  Umoja  wa  Ulaya, hilo  bado  halijaondolewa  na ushindi  wa  jana. Lakini uungwaji  wake  mkono  unatosha kuweza kuendelea  kujaribu  kufikia  makubaliano  baina  ya  London  na Brussels, kwa  njia  yoyote  ile  ili  kuweza kupata  wingi  kwa  ajili ya  makubaliano  ya  Brexit. May  ameonesha , kwamba  ni  imara na  mwanamke wa  shoka  kuliko wakosoaji  wake  walivyofikiria.

Gazeti  la  Volksstimme  la  mjini  Magdeburg  likiandika  kuhusu  kura hiyo  ya  kutokuwa  na  imani  bungeni  jana  mjini  London, linaandika:

Imeonekana, Theresa May anaweza  pia  kushinda. Wabunge wakorofi  wa  chama  cha  Conservative , Tories, ambao  walitaka kumfurusha  kwa  kutumia  kura  ya  kutokuwa  na  imani  nae, wameshindwa. May  anaendelea   kuwa  madarakani  kama  kiongozi wa  chama  pamoja  na  waziri  mkuu. Pamoja  na  hayo  kwa kiongozi  huyo  hii  ni ushindi  wa  taabu  sana. Unapoanza  mkutano wa  Umoja  wa  Ulaya  leo , anaonekana  May  baada  ya  ziara yake  katika  miji  mikuu  ya  mataifa  ya  Ulaya  kwamba  uwezo wake  wa upatanishi  umepunguzwa. Mataifa  ya  Ulaya  hayako tayari  kuidhinisha  hatua  ya kubadilisha suala  la  mpaka  wa Ireland ya  kaskazini . Huenda  mabadiliko kidogo ya lugha tu  ndio huenda  yanawezekana. Kwa  jumla  waziri  mkuu  hatakuwa  na uwezo  wa  kubadili hali  ya  kupinga  makubaliano  hayo  ya  Brexit.

Mhariri  wa  gazeti  la  Rheinpfalz  la  mjini  Ludwigshafen  akiandika kuhusu  shambulio  la  kigaidi  mjini  Strasbuorg  anaandika:

Hapa Ujerumani  huenda  pengine  baadhi  ya  watu  walifikiri, kwamba ugaidi  wa  wapiganaji  wa  jihadi  umekwisha, tangu  pale kundi  linalojiita  Dola  la  Kiislamu  nchini  Iraq  na  Syria  kwa  kiasi kikubwa  waliposhindwa. Nchini  Ufaransa  hakuna  anayefikiria hivyo. Shambulio  katika  mji  wa  Strasbourg  ni  la  tatu  mwaka  huu katika  ardhi  ya  Ufaransa, na  la  tano  katika  wakati  wa  utawala wa  rais Emmanuel Macron. Katika  utafiti  wa  kituo  cha  tathmini ya  ugaidi  nchini  Ufaransa  kati  ya  mwaka  2013  na  2016 nchi hiyo imekuwa  ikikabiliwa  zaidi  na  mashambulizi  ya  aina  hiyo duniani. Katika  nchi  hiyo  mtandao  wa  wana  jihadi  uko  imara zaidi, ndani  na  nje  ya  nchi  hiyo. Watafiti wanasema  kuna Wafaransa   maelfu  kadha  ambao  wako  tayari  kufanya mashambulizi.

Bado  katika  mada  hiyo  mhariri  wa  gazeti  la  Suedkurier anaandika:

Mtu  huyo alikuwa  anafahamika  na  polisi  na  ana rekodi  ya uhalifu. Yumo  katika  orodha  ya  Waislamu  hatari wenye  itikadi kali. Alipaswa  kukamatwa, lakini  maafisa  hawakumpata  na  sasa ndio  wanamtafuta. Baada  ya  shambulio  mjini  Strasburg  linarejea tena  swala  la  zamani  likiwa  na dharura  mpya. Kwa nini mataifa ya  kidemokrasia  yanashindwa  kufawajibu wao  kila  wakati , wahalifu  kama  hao kuwazuwia , nchini  Ufaransa  na  hata  hapa Ujerumani?

Nae  mhariri  wa  gazeti  la  Emder Zeitung  anazungumzia  kuhusu mkutano  wa  Umoja  wa  mataifa  wa  mazingira  nchini  Poland. Mhariri  anaandika.

Kesho unamalizika  mkutano  huo. Kwa  bahati  mbaya, kunakuja  kile ambacho  hadi  sasa  tumekisikia  katika  mkutano  wa  mazingira, kile  tunachokifahamu  kila  mmoja. Baada  ya  miito ya  kina kwamba ni  muhimu  kiasi  gani  kufikia  makubaliano yenye  manufaa, inashindikana  kwa  mara  nyingine  tena  kupata  ushauri  imara. Masuala  muhimu  yanayoleta  vizuwizi  bado  hayajatatuliwa, alisema  katibu  mkuu  wa  Umoja  wa  mataifa  Antonio Guterres jana. Hali  hii  si  nzuri kabisa. Mtu  hapaswi  hata  hivyo  kukata tamaa, lakini  ni  wazi  kwamba  hatari  ni  kubwa, kwamba  jumuiya ya  kimataifa  bado  ina  nafasi ya  mwisho, kuzuwia  mabadiliko  ya tabia  nchi  ambayo  hayajazuiliwa na  yameachwa  kusambaa.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / Inlandspresse

Mhariri: Josephat Charo