1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini: Waranti kukamatwa mkuu wa zamani wa Volkswagen

Sekione Kitojo
7 Mei 2018

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha na mada kuhusu waranti wa kukamatwa mkuu wa zamani wa kampuni  ya Volkswagen,maandamano dhidi ya Putin,na matamshi ya rais wa Marekani akikejeli mauaji nchini Ufaransa.

https://p.dw.com/p/2xIY8
Martin Winterkorn - Volkswagen
Martin Winterkorn mkuu wa zamani wa kampuni ya VolkswagenPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Sohn

Mhariri  wa  gazeti  la Nordwest-Zeitung  la  mjini Oldenburg , akiandika  kuhusiana na  waranti uliotolewa ili  kukamatwa kwa mwenyekiti  wa  zamani  wa  kampuni  ya  Wolkswagen Martin Winterkorn anaandika  kwamba msukumo wa  hivi  sasa  dhidi  ya mkuu  huyo  wa  zamani  wa Volkswagen unawaweka wachunguzi wa  Ujerumani  katika  mbinyo  mkubwa kuwa wazi. Mhariri anaendelea.

"Wamarekani wanatakiwa pengine  kuangalia upya msingi  wa mashitaka  yao. Walifikia  karibu  sana  na  kumshitaki, kwa  kuwa Winterkorn  aliongoza  kampuni  hiyo na kuangalia  kila  shughuli iliyokuwa  ikifanyika,  katika  utendaji  wa  hivi  sasa  na  pia  hapo kabla na  kwamba  alifahamu  udanganyifu  uliokuwa  ukifanyika na pia  hakuzuwia   ama  kupinga  hatua  hizo."

Kama  hali  hiyo  ni  sahihi, mkuu  huyo  wa  kampuni  hiyo ameshiriki katika  hatua za  kutengeneza  vifaa  ambavyo  si  sahihi, basi anakabiliwa  na muanguko  mkubwa.

Kuhusu  mada  hiyo  hiyo  mhariri  wa  gazeti  la Badische Neueste Nachrichten  anaandika  kwamba mzozo mkuu  hata  hivyo  si  kati ya  Martin Winterkorn, Volkswagen  na mahakama: Mhariri anaandika:

"Hapana, mzozo  huu  ni  baina  ya  mamilioni  ya  watu  wanaomiliki magari  yanayotumia  mafuta  ya  dizeli  kutoka  katika  kampuni  hiyo ya  Volkswagen, ambao  wanakabiliwa  na  kitisho  cha  kuzuiwa kuendesha  magari  hayo. Volkswagen kama  kampuni  kwa  hali  hii inamakosa."

Gakuba:

Mhariri  wa  gazeti  la Stuttgarter Zeitung  anazungumzia  kuhusu maandamano  nchini  Urusi  dhidi  ya  rais Vladimir  Putin. Mhariri anandika:

"Miaka  sita  iliyopita  mamia  kadhaa  ya  waandamanaji  nchini Urusi  walimiminika  katika  mitaa  ya  mji mkuu  wa  nchi  hiyo. Lakini maandamano  hayo sasa ni  tofauti. Ni  tofauti  na  yanapungua  kasi , kwasababu  wenye  madaraka  nchini  Urusi  hivi  sasa  wanaona kutumia  nguvu ndio jambo  muhimu  ili  kuzuwia watu kudai yale wanayoyaona  kuwa  ni  sahihi. Yanaporomoka  pia  kwa sababu upinzani  haufahamu  ni mpango  gani  hasa  wanaweza kuuwasilisha kwa  wananchi, mbali  na  suluhisho  la kauli  mbiu  ya  " Urusi  bila ya  Putin".  Serikali  ya  Urusi  ingeweza kutoa  haki  ya waandamanaji  kukusanyika. Ingeweza kujisikia  vizuri, kwa  kuwa rais  wa  Urusi  anaungwa  mkono  kwa  asilimia  80  na  wananchi. Lakini  haifanyi  hivyo , kwa  kuwa  asilimia  hii  80  kwa  kweli  ni matunda  ya   vitisho, ambavyo  vimeendelea  kwa  matumizi  ya nguvu  kubwa."

Nae  mhariri  wa  gazeti  la  Fränkischer Tag , la  mjini  Bamberg anazungumzia  kauli  ya  rais  wa  Marekani  Donald Trump  kuhusu kejeli  alizofanya  rais  huyo  kwa  mauaji  ya  kigaidi  nchini Ufaransa. Mhariri  anaandika:

"Rais  wa  45  nchini  Marekani  Donald Trump  kwa  mara  nyingine tena  ametumia  maneno  ya  kejeli  alipokuwa  katika  mkutano  na chama  cha  wamiliki  silaha  chenye  ushawishi  mkubwa  nchini Marekani  na  ambacho  kilichangia  kiasi  cha  dola  milioni 30 katika  kampeni  za  uchaguzi  mkuu  wa  Marekani. Rais  ambaye anaweza  kununuliwa. Rais  ambaye  ana  damu  katika  mikono yake."

Hayo  ni  baadhi  ya  maoni  ya  wahariri  wa  magazeti  ya  hapa Ujerumani , kama  yalivyokusanywa  na  Sekione Kitojo:

Mwandishi: Sekione Kitojo / Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman