1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Walter Lausch11 Machi 2008

Katika maoni yao leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanachambua mtazamo wa mwenyekiti wa chama cha SPD Kurt Beck juu ya chama cha mlengo wa shoto.

https://p.dw.com/p/DMX9
Mwenyekiti wa chama cha SPD kilichomo katika serikali ya mseto Ujerumani Kurt BeckPicha: picture-alliance/dpa


Mwenyekiti wa chama cha Social Demokratik, kilichomo katika serikali ya mseto  nchini Ujerumani, bwana Kurt Beck anakabiliwa  na  mgogoro ndani ya chama  chake kutokana na msimamo wake juu ya chama cha wakomunisti wa zamani.


Juu ya  hayo mhariri wa gazeti la STUTTGARTER  anasema katika maoni yake kuwa licha  ya kurejea tena kwenye jukwaa  la kisiasa baada ya kuugua kwa siku mbili tatu, yeye pamoja na mjumbe wa chama cha SPD aliesimama katika uchaguzi wa  jimbo la kati la Ujerumani ,Hesse, Andrea Ypsilanti  wamemalizika kisiasa.

Gazeti linasema Kurt Beck na Ypsilanti wametia dosari uadilifu wao kutokana na simamo wao juu ya chama cha mlengo wa kushoto cha wakumunisti wa zamani.

Mhariri anasema ni kweli kwamba baraza kuu la chama cha Social demokratik linamwuunga mkono bwana Beck, lakini  kisiasa bado hajapata afuaeni.

Kutokana na msimamo wake juu ya chama hicho cha wakomunisti wa zamani, wanachama wengi wa SPD wanataka kujua chama chao sasa kinaelekea wapi?

Hatahivyo mhariri wa gazati la NORDBAYERISCHE KURIER anasema hata mwenyekiti wa chama anaweza kufanya kosa lakini hana budi akiri kuwa amefanya kosa badala ya kujaribu kubabaisha watu.

Mwenyekiti Beck alikuwa na fursa ya kujirekebisha, lakini amepoteza fursa hiyo na yumkini pia amepoteza  fursa ya kugombea  ukansela  mwaka kesho.


Gazeti la FRANFURTER RUNDSCHAU linasema, licha ya kinachoonekana kuwa mgogoro ndani ya chama chake, mwenyekiti Beck bado anadhibiti hatamu na ataendelea kukiongoza chama hicho.

Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kwa kusema kuwa bwana Beck hana njia nyingine ila kuendelea kukiongoza chama chake-sababu ni kwamba katika uongozi wa SPD  hakuna  mbadala; kwa sasa  hakuna  tena mtu mwengine  wa kushika usukani wa uongozi.Wapinzani wake wa ndani hawana ujasiri wa kumkabili.

Pamoja na hayo Kurt Beck anaungwa mkono na mashina ya chama ,licha ya kosa alilofanya - kuashiria utayarifu wa kushirikiana na chama cha wakomunisti wa zamani.

Mhariri wa gazeti la TRIERISCHEN VOLKSFRUEND anasema bwana Beck ameonesha ukakamavu na roho ngumu katika mgogoro unaomkabili lakini haina maana kwamba haiwezekani kupatikana mtu mbadala katika uongozi wa chama SPD.

Gazeti la LANDESZEITUNG linauliza iwapo ni uhalifu kuvunja ahadi katika siasa?

Mhariri wa gazeti hilo anajijibu mwenyewe kwa kusema hapana, la sivyo wanasiasa wote wangelikuwa wahalifu.

Anasema wakati mwingine ni jambo la lazima kuvunja ahadi,mradi hayo yanafanyika wakati mujarab.