1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHaiti

Magenge yenye silaha nchini Haiti yataka serikali ipinduliwe

Mohammed Khelef
20 Septemba 2023

Magenge yenye silaha Haiti yashinikiza serikali ya Waziri Mkuu Ariel Henry, kuondolewa madarakani.

https://p.dw.com/p/4WbzE
Suala hilo la Haiti ni sehemu ya mazungumzo ya pembezoni baina ya Rais Biden na mwenzake wa Brazil, Inacio Lula da Silva, ambayo yamefanyika Jumatano jijini New York.
Suala hilo la Haiti ni sehemu ya mazungumzo ya pembezoni baina ya Rais Biden na mwenzake wa Brazil, Inacio Lula da Silva, ambayo yamefanyika Jumatano jijini New York.Picha: Odelyn Joseph/AP Photo/picture alliance

Siku moja baada ya Rais Joe Biden wa Marekani kuuomba Umoja wa Mataifa kuidhinisha kikosi cha kimataifa kurejesha amani nchini Haiti, magenge yenye silaha nchini humo yametowa wito wa kupinduliwa kwa serikali.

Shinikizo la kimataifa linazidi kuongezeka kwa Umoja wa Mataifa kuridhia kikosi maalum cha walinda usalama kupelekwa nchini Haiti ili kurejesha udhibiti wa mamlaka katika taifa hilo masikini kabisa kwenye ukanda wa Karibiani ambalo linakabiliwa na magenge yenye silaha.

Kwenye hotuba yake kwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa hapo jana, Rais Biden alitowa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja huo kuharakisha kutumwa kwa kikosi hicho, ambacho tayari Kenya imeshaonesha utayari wa kutoa maafisa wa usalama:

Mmojawapo wa viongozi wa makundi yenye silaha, Jimmy "Barbecue" Cherizer, ametowa wito kwa raia wa kisiwa hicho kuingia mitaani kwa maandamano ya kuiangusha serikali ya Waziri Mkuu Ariel Henry
Mmojawapo wa viongozi wa makundi yenye silaha, Jimmy "Barbecue" Cherizer, ametowa wito kwa raia wa kisiwa hicho kuingia mitaani kwa maandamano ya kuiangusha serikali ya Waziri Mkuu Ariel HenryPicha: Odelyn Joseph/AP Photo/picture alliance

"Ninaliomba Baraza la Usalama liidhinishe kikosi hiki sasa. Watu wa Haiti hawawezi kungoja tena," alisema Biden.

Suala hilo la Haiti ni sehemu ya mazungumzo ya pembezoni baina ya Rais Biden na mwenzake wa Brazil, Inacio Lula da Silva, ambayo yamefanyika Jumatano jijini New York.

Mambo yazidi kuharibika Haiti

Lakini wakati juhudi hizo zikiendelea, ndani ya Haiti kwenyewe mambo yanazidi kuharibika.

"Kila geto litashuka mtaani kila siku na hatuna chochote cha kuuficha ulimwengu. Wote wanajuwa kuwa tuna silaha. Sio kwamba tunahamasisha kupambana na Ariel Henry pekee, lakini pia tunahamasisha watu. Vita vyetu vitakuwa pia vya silaha dhidi ya Ariel Henry," amesema Jimmy "Barbecue" Cherizer, Mmojawapo wa viongozi wa makundi yenye silaha.

"Barbecue", ambaye ni afisa wa zamani wa polisi anayeongoza sasa muungano wenye nguvu wa magenge yanayodhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu wa nchi hiyo, Port-au-Prince, aliwaongoza mwenyewe maelfu ya wapiganaji wake wenye silaha katika mitaa ya mji huo mkuu, huku wakipiga ngoma na kuziba barabara.

Magenge ya wahalifu yawahangaisha raia Haiti

Magenge yenye silaha haiti yazidi kujiimarisha

Magenge ya Haiti, ambayo mara kadhaa hukabiliana na polisi kwa silaha na yanayofaidika na shughuli haramu kama vile mauaji na ulanguzi wa madawa ya kulevya, yamepata nguvu sana tangu alipouawa Rais Jovenel Moise mwaka 2021.

Mauaji hayo yalisababisha ombwe la madaraka na tangu wakati huo Waziri Mkuu Ariel Henry amekuwa akitawala kama kiongozi wa kipindi cha mpito.

Henry ameahidi kuwa ataitisha uchaguzi baada ya hali ya usalama kuimarika na amekuwa akiomba msaada ya jumuiya ya kimataifa kukabiliana na magenge hayo.

Vyanzo: Reuters, AFP