1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaahirisha uamuzi kesi ya wapenzi wa jinsia moja

Mohammed Khelef
22 Februari 2019

Mahakama Kuu ya Kenya imeahirisha hukumu iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu juu ya uhalali wa sheria inayoharamisha mahusiano ya kimapenzi ya watu wa jinsia moja. Mmoja wa majaji wa mahakama hiyo, Chacha Mwita, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa bado majalada ya kesi hiyo ni mengi na wanayafanyia kazi na uamuzi rasmi utatolewa tarehe 24 Mei mwaka huu.

https://p.dw.com/p/3DqEg

Mahakama Kuu ya Kenya iliahirisha siku ya Ijumaa (22 Januari) uamuzi uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu juu ya ama nchi hiyo iendelee na sheria inayoharamisha mapenzi ya jinsia moja au iifute sheria hiyo iliyorithiwa kutoka utawala wa kikoloni.

Hatua hiyo ilipokelewa kwa fadhaa na baadhi ya wanachama wa jumuiya ya wapenzi wa jinsia moja na washirika wao, ambao wamekuwa wakingojea kwa hamu uamuzi juu ya ombi walilowasilisha mahakamani miaka mitatu iliyopita.

"Majalada yamenizidi kimo... bado tunayafanyia kazi," alisema Chacha Mwita, mmoja wa majaji wa Mahakama Kuu, ambaye aliongeza kuwa mmoja wa majaji wenziwe yuko likizo na kwamba jopo la majaji watatu linashughulika na kesi nyengine nyingi.

Alisema uamuzi unapangwa kuwa Mei 24.

"Tunapanga kukutana mwezi Aprili ikiwa kila kitu kitakwenda vyema na tutaangalia uwezekano wa kufikia uamuzi. Hamuonekani kuwashukuru majaji kwa kazi kubwa wanayofanya."

Sheria inayopingwa

Namibia Gay Pride Parade 2016
Wanaharakati wanataka sheria ya enzi ya ukoloni kufutwa kwa kuwa ni kinyume na katiba.Picha: picture-alliance/NurPhoto/O. Rupeta

Mashirika yanayopigania haki za wapenzi wa jinsia moja yanaitaka mahakama kuondoa vipengele viwili vya sheria ya jinai ambavyo vinayafanya mapenzi ya jinsia moja kuwa uhalifu. 

Kipengele kimoja kinasema kuwa yeyote mwenye "uelewa usiofaa dhidi ya maumbile" anaweza kufungwa hadi miaka 14 jela. Chengine kinatoa hukumu ya kifungo cha miaka mitano kwa "matendo yasiyo heshima baina ya wanaume."

Katika mitandao ya kijamii, wapenzi wa jinsia moja na washirika wao wamekuwa wakizihesabu siku na saa kuelekea uamuzi huo.

"Kusema kuwa tumefadhaishwa kutakuwa ni kuidogosha," liliandika Baraza la Haki za Binaadamu za Wapenzi wa Jinsia Moja (NGLHRC) kwenye ukurasa wake wa Twitter. Baraza hilo ni moja ya waliopeleka kesi hiyo mahakamani. 

Patrick Gathara, mchambuzi wa masuala ya kijamii, aliita hii kuwa siku ya huzuni kwa mahakama. Hata hivyo, Douglas Masinde kutoka Kilifi, pwani ya Kenya, aliiambia DW kwamba uamuzi wa kuahirisha kesi unawapa muda wao, kama jamii ya wapenzi wa jinsia moja, kurudi kwa jamii kuwaeleza umuhimu wa hukumu hiyo kwao kabla ya kutolewa.

Wanaharakati wanaamini kuwa Kenya inayo nafasi ya kuiongoza Afrika kwa kuachana na sheria ambazo zinafanya chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja kuwa kubwa katika jamii zenye sheria kama hizo kwa zaidi ya nusu karne sasa. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga