1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya ECHR yasema chanjo za lazima huenda zikahitajika

8 Aprili 2021

Mahakama ya Haki za Binaadam ya Ulaya ECHR kwa mara ya kwanza imetoa uamuzi wa kuzingatia suala la uchomaji chanjo kwa lazima. Hukumu hii huenda ikawa na mchango muhimu katika juhudi za kumaliza janga la COVID-19.

https://p.dw.com/p/3rkJC
Brasilien Impfung gegen Gelbfieber
Picha: Fabio Teixeira/AA/picture alliance

Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binadamu (ECHR) huko Strasbourg siku ya Alhamisi iliamua kwamba chanjo za lazima hazitakiuka sheria za haki za binadamu na huenda zikawa muhimu katika jamii za kidemokrasia.

Uamuzi huu unajiri baada ya kumalizika kwa malalamiko yaliyowasilishwa kortini na familia kutoka Jamhuri ya Czech kuhusu chanjo za lazima kwa watoto.

Ingawa uamuzi huo haukushughulikia moja kwa moja chanjo dhidi ya COVID-19, wataalamu wanaamini unaweza kuwa na athari kwa juhudi za utoaji chanjo dhidi ya virusi vya corona, hususan kwa wale ambao hadi sasa wamekataa kukubali kuchanjwa.

Hukumu hii "inaimarisha uwezekano wa chanjo ya lazima wakati huu wa janga la COVID-19," alisema Nicolas Hervieu, mtaalamu wa sheria aliyebobea katika mahakama ya ECHR, alipozungumza na shirika la habari la AFP.

Je! Uamuzi wa korti ulikuwa juu ya nini?

Uamuzi wa Mahakama umesema kwamba chanjo za lazima zinazosimamiwa na maafisa wa afya wa nchini Czech zilikuwa zinaendana na "maslahi bora" ya watoto. Lengo ni kuwa kila mtoto analindwa dhidi ya magonjwa, kupitia chanjo au kwa kinga," ripoti hiyo ilisema.

Mahakama imepitisha kwamba sera ya Jamhuri ya Czech haikiuki kifungu cha nane cha sheria kuhusu haki ya kuheshimu maisha ya faragha kwa mujibu wa sheria za Ulaya kuhusu haki za binadamu.

Tschechien Brno | Impfzentrum
Kituo cha chanjo cha Brno kikitoa chanjo ya Pfizer/BioNTech kwa walimu wa shule ya Svazna, Jamhuri ya CzechPicha: Vaclav Salek/Ctk/dpa/picture alliance

Kwa mujibu wa sheria za Czech watoto sharti wadungwe chanjo dhidi ya magonjwa tisa yakiwemo mkamba, pepopunda, mafua, homa ya ini na ukambi.

Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani na familia ambazo zilikuwa zimetozwa faini au ambazo watoto wao walikuwa wamekatazwa kwenda katika shule ya chekechekea kwa kushindwa kutimiza masharti ya chanjo kwa mujibu wa sheria.

Hukumu ya mfano kwa juhudi za utoaji chanjo

Mataifa kote Ulaya yamesuhudia ongezeko la taarifa zisizo sahihi kuhusu janga la virusi vya corona. Hii imepelekea watu sio tu kutilia shaka kirusi chenyewe cha corona, bali pia kuhusu chanjo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.

Watu wanaokataa kudungwa chanjo, au kuwaruhusu watoto wao wadungwe chanjo wameeneza mitazamo tofauti tofauti kuhusu kwa nini serikali zinataka umma uchanjwe.

Matokoe yake serikali huenda zinakabiliana na idadi kubwa ya makundi ya watu katika jamii ambao hawataki kudungwa chanjo, hivyo kulifanya lengo la kujenga kinga imara mwilini dhidi ya corona kuwa vigumu kufikiwa.

Ingawa hukumu ya mahakama ya haki ya Ulaya huenda imeweka mfano kwamba chanjo za lazima haikiuki sheria ya haki ya Ulaya, hii haina maana mataifa ya Ulaya yatawalazimisha raia wao wadungwe chanjo.