1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama yamzuwia kutumia mitandao kwa miaka 8

Mohammed Khelef
11 Januari 2017

Mahakama ya kupambana na ugaidi nchini Saudi Arabia imeibakisha hukumu ya kifungo cha miaka minane na kisha marufuku ya miaka mingine minane ya kutotumia mitandao ya kijamii dhidi ya mwanaharakati, Abdulaziz al-Shubaily.

https://p.dw.com/p/2Vd7i
Saudi-Arabien König Salman bin Abdulaziz Al Saud
Picha: picture-alliance/dpa/Saudi Press Agency

Kituo cha Haki za Binaadamu cha Ghuba kinachoongozwa na Shubaily kimesema kwenye taarifa yake kuwa hukumu hiyo iliyotolewa jana Jumanne (10 Januari 2017) "ni sawa na ile aliyopewa mwezi Mei", lakini mwanaharakati huyo haitambui mahakama hiyo kwa kuwa inajishughulisha na makosa ya ugaidi.

Mahakama ya rufaa iliirejesha kesi hiyo kwenye "Mahakama Maalum ya Uhalifu" kwa mapitio zaidi. 

"Shubaily amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kudai mageuzi na kuwatetea watu wanaovunjiwa haki zao kwenye taifa ambalo linatawaliwa na mfumo wenye itikadi kali za kihafidhina," kilisema kituo hicho.

Mwanaharakati huyo alikuwa kiongozi wa Taasisi ya Haki za Kiraia na Kisiasa ambayo ilivunjwa na mahakama mwaka 2013.

Alikuwa wa mwisho katika wanachama wa kundi hilo kufungwa, kwa mujibu wa shirika la haki za binaadamu la Amnesty International, ambalo limelaani kile linachokiita "matumizi ya kikatili na kikandamizaji ya sheria za kupambana na ugaidi."

Kituo cha Haki za Binaadamu cha Ghuba kimesema hukumu dhidi ya Shubaily "ambayo ilitolewa baada ya dhihaka ya kisheria isiyofuata vigezo vya kimataifa wala halali, ni sehemu ya tabia inayoendelea ya mamlaka za nchi."

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo