1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maharamia wakisomali wadai dola millioni 25 kabla ya kuiachilia huru meli ya Saudi Arabia

21 Novemba 2008

Marekani na Saudi Arabia hazijathibitisha taarifa hizo

https://p.dw.com/p/FzEe
Uharamia katika Pwani ya Somalia wazusha hofu kwa jumuiya ya kimataifaPicha: AP

Jeshi la majini la Marekani pamoja na wahusika wa meli ya mafuta ya Saudi Arabia iliyotekwa nyara na maharamia wakisomali hawajathibitisha taarifa zilizotolewa hii leo kwamba watekaji nyara hao wameitisha kiasi cha dolla milioni 25 ili waiachilie meli hiyo.

Kwa upande mwingine kufuatia kuchacha kwa opresheni za maharamia katika pwani ya eneo la Afrika mashariki kampuni kubwa ya meli za kusafirishia mafuta iliyo na makao yake mjini Oslo imesema njia pekee ya kupambana na hali hiyo ni kuchukuliwa hatua za kijeshi.Mwezi uliopita jumuiya ya kujihami ya nchi za magharibi Nato ilituma meli za kivita katika ghuba ya Aden katika harakati za kupambana na uharamia huku Umoja wa Ulaya pia ukitarajiwa kuanzisha opresheni za kukabiliana na hali hiyo katika pwani ya Somalia desemba 8.

Msemaji wa kampuni ya kimataifa ya Vela yenye makao yake Duabai na ambayo ni tawi la kampuni ya Saudi Arabia ya Aramco amesema hadi kufikia wakati huu hawajapata taarifa zozote mpya kuhusiana na suala la maharamia kuitisha fedha na kutokana na hilo amekataa kuzungumzia chochote.

Vela ni kampuni inayoendesha shughuli za meli ya Sirius Star ambayo inamilikiwa na kampuni ya Saudi Arabia ya Aramco.Meli hiyo kubwa kabisa iliyo na uwezo wa kubeba mapipa millioni mbili ya mafuta ilitekwa nyara na maharamia kiasi wiki moja iliyopita.

Shirika la habari la ufaransa la AFP jana limemnukuu mmoja wa maharamia hao wa kisomali akisema kwamba wanachokitaka ili kuiachilia meli hiyo ni dolla milioni 25 na pia wameshatoa muda wa mwihso wa fedha hizo kutolewa ambao ni siku 10.

Wakati huohuo wataalamu wanasema kwamba kutokana na kuzidi kuongezeka nguvu kwa uharamia katika eneo hilo majeshi ya kimataifa yanajizatiti kutafuta mbinu mpya kwasababu huenda matrumizi ya nguvu yasifue dafu.Aidha kukithiri kwa visa vya uharamia katika pwani ya Somalia shirika la kimataifa linalohusika na safari za baharini la IMB limetoa mwito wa usaidizi katika kukabiliana na hali hii.

Meli kadhaa zinaendelea kushikiliwa katika pwania ya Somalia na maharamia. Mwenyekiti wa kamati ya kijeshi ya jumuiya ya nchi za magharibi Nato bwana Di Paola anasema kwamba Kasi ya uharamia katika eneo hilo imefikia katika kiwango ambacho kinamshangaza kila mmoja.Aidha kwa upande wake Ujerumani imesikitishwa na hali inavyozidi kuwa mbaya katika eneo hilo.

Akiulizwa kuhusu uwezekano wa ujerumani kushiriki katika harakati za kupambana na uharamia kwenye pwani ya Somalia waziri wa ulinzi wa Ujerumani Franz Joseph Jung alisema,

''Hilo ni suala linalozungumzwa katika katiba.Kupambana na uharamia ni jukumu la polisi na jeshi la Ujerumani linataka kuchukua kazi hiyo basi lazima paweko utaratibu maalum wa pamoja kuhusu usalama.Hii ina maana patahitajika kibali cha kimataifa.kwa kufafanua zaidi kibali cha Ulaya kitahitajika na nahitaji idhini ya bunge la Ujerumani Bundestag.''

Jumuiya ya Nato ilituma meli nne za kivita katika ghuba ya Aden mwezi uliopita kukabiliana na uharamia pamoja na kusindikiza meli za misaada wakati Umoja wa Ulaya ukitajariwa kutuma majeshi yake desemba 8.Miongoni mwa nchi ambazo tayari zimepeleka meli za kivita katika eneo la kuingilia bahari ya Sham ambayo ni muhimu katika biashara ya kimataifa ni Ufaransa,India,Korea Kusini,Urussi,Uhispania na Marekani.

Tayari kampuni kubwa inayohusika na meli za kusafirisha mafuta iliyo na makao mjini Oslo imesema kwamba njia pekee ya kuukomesha uharamia kattika pwani ya Somalia ni kutumia nguvu za kijeshi.Kampuni hiyo ambayo ina meli 80 inafikiria uwezekano wa kuzigeuza meli zake kuelekea eneo hilo na ghuba ya Aden ikiwa jumuiya ya kimataifa haitatumia nguvu.

Pamoja na yote lakini wadadisi wa mambo wanasema ili jumuiya ya kimataifa kuweza kupunguza kasi ya uharamia huenda ikabidi kugeukia njia ya kuanzisha hujuma za kushtukiza lakini wanaonya kwamba uharamia utaendelea na unafuu utakuwa tu wa muda mfupi.