1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahasimu Yemen wakubaliana kuondoa wapiganaji Hodeida

Iddi Ssessanga
18 Februari 2019

Umoja wa Mataifa unasema pande hasimu nchini Yemeni zimekubaliana juu ya hatua ya kwanza ya kuondoa vikosi kutoka mji wa bandari wa Hodeida, kufuatia mkutano wa siku mbili ulioihusisha serikali na waasi wa Kihouthi.

https://p.dw.com/p/3DZN5
Jemen Rebellen werden sich an Bord eines UN-Schiffes treffen
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Mohammed

Uhamishaji wa wanajeshi kutoka Hodeida ni mojawapo ya masharti ya mapatano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Desemba nchini Sweden, yanayotoa wito kwa serikali na Wahouthi kuondoa vikosi vyao kutoka bandari na baadhi ya sehemu za mji huo.

Baada ya siku mbili za mazungumzo mjini Hodeida, serikali na Wahouthi walikamilisha makubaliano kuhusu awamu ya kwanza ya uondoaji huo na pia walikubaliana kimsingi juu ya awamu ya pili, kulingana na taarifa ya Umoja wa Mataifa.

Mazungumzo hayo yaliongozwa na Jenerali kutoka Denmark Michael Lollesgaard kama mwenyekiti wa kamati ya kuratibu uhamishaji wa wapiganaji (RCC), inayowajumlisha wajumbe wa serikali pamoja na Wahouthi.

Jemen Hodeida Regierungstruppen rücken vor
Wapiganaji wa wanaoiunga mkono serikali ya Yemen wakisonga mbele kuelekea eneo la bandari ya Hodeida mwishoni mwa 2018.Picha: Getty Images/AFP

Pande hizo zilipiga hatua muhimu kuhusu mipango ya uhamishaji wa vikosi lakini hakuna tarehe ilioafikiwa kuanza zoezi hilo.

Awamu ya kwanza inahusu kuondolewa kwa wapiganaji kutoka bandari za Hodeida, Saleef, Ras Issa na kutoka maeneo ya mji kuliko na miundombinu ya kibinadamu.

Chini ya makubaliano ya Stockholm, uondoaji wa vikosi ulipaswa kufanyika wiki mbili baada ya usitishaji mapigano kuanza Desemba 18, lakini muda huo haukuheshimiwa.

Mapigano madogomadogo yaendelea

Mapatano ya Hodeida yametekelezwa kwa sehemu kubwa lakini mapigano madogo madogo yanaendelea kati ya Wahouthi na mahasimu wao katika muungano unaoongozwa na Saudi Arabia unaopambana kurejesha udhibiti wa serikali inayotambuliwa kimataifa.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa ilisema pande hizo mbili zilikubaliana kimsingi kuhusu awamu ya pili, inayohusisha uondoaji kamili wa wapiganaji wa pande zote kutoka mkoa mzima wa Hodeida kulingana na mpango wa Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa unatumai kuwa kupungua kwa uhasama mjini Hodeida kutaruhusu mahitaji  muhimu ya chakula na dawa kuwafikia mamilioni ya watu wenye uhitaji nchini Yemen.

Martin Griffiths UN Sonderbeauftragter Jemen
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Martin Griffiths ataripoti kwenye baraza la usalama kuhusu maendeleo yaliofikiwa.Picha: picture-alliance/Keystone/S. Di Nolfi

Bandari hiyo ya bahari ya Sham ni njia muhimu ya uingizwaji wa bidhaa na msaada nchini Yemen, ambayo Umoja wa Mataifa umeielezea kama mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.

Mazungumzo hayo ya Jumamosi na Jumapili ndiyo yalikuwa ya nne kufanyika kujaribu kufikia muafaka kuhusu utaratibu wa uondoaji wa vikosi tangu mapatano ya kusitisha mapigano yalipoanza kutekelezwa Desemba 18.

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Martin Griffiths, alieongoza makubaliano ya Stockholm, anatarajiwa kuripoti kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne juu ya maendeleo hayo.

Karibu watu 10,000 wameuawa katika vita hivyo, kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani WHO, lakini mashirika ya haki za binadamu yanasema idadi ya vifo ni kubwa zaidi ya hapo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe,ape

Mhariri: Daniel Gakuba