1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Uturuki yaimarisha mashambulizi ngome ya IS Syria

Jane Nyingi23 Agosti 2016

Kwa siku ya pili mfulululizo majeshi ya Uturuki yameendelea kuyashambulia maeneo ya mpakani yanayodhibitiwa na wapiganaji wa dola la kiislamu IS nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1JnTR
Syrien Türkische Luftangriffe auf die kurdische PKK
Picha: picture-alliance/AA

Hatua hiyo ni katika kuyajibu mashambulizi yanayofanywa na kundi hilo la IS tukio la hivi karibuni likiwa mashambulizi ya makombora mawili yaliyolenga mji wa Karkamis ulio kusini mashariki mwa Uturuki.

Mashambulizi hayo na majeshi ya Uturuki yalilenga maeneo manne ya mji huo yakiwemo yale ya chama cha wapigaji wa kikurdi cha Democratic Union. Harakati hizo na Uturuki zinawadia siku chache baada ya IS kushtumiwa kufanya shambulizi la bomu la kujitoa mhanga katika mji wa Gaziantep ulio kusini mwa Uturuki.

Shambulizi hilo katika hafla ya harusi lilisababisha vifo vya watu 54 wengi wao wakiwa watoto na vijana, 28 miongoni mwao wakiwa chini ya umri wa miaka 18 huku karibu 22 wakiwa chini ya miaka 14. Eneo hilo la Gaziantep ni kitovu cha wakimbizi waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe vya zaidi ya miaka mitano nchini Syria.

Türkei Explosion bei Hochzeit in Gaziantep
Jamaa za walioshambuliwa katika halfa ya harusi,GaziantepPicha: Getty Images/AFP

Awali Uturuki ilisema mtoto asiyepindukia miaka 15 ndiye aliyefanya shambulizi hilo, kufuatia kile kinachoaminika ni kufuata maagizo ya wapiganaji wa kundi hilo la IS. Hata hivyo saa chache baadae waziri mkuu Binali Yildirim alibadili kauli hiyo na kusema taarifa hizo zilikuwa za kupotosha na hadi sasa hawafahamu aliyefanya shambulizi hilo. "Kuhusu shambulizi hilo,bila shaka ni mlipuko mkubwa. Hadi sasa hatujaweza kupata ishara zozote kuhusu muhusika,taarifa zilizotolewa awali zilitokana na ushahidi uliotolewa na walioshuhudia mlipuko huo. Vinginevyo si sahihi kuweka dhana ya mapema kuhusu aliyefanya shambulizi hilo au ni shirika lipi. Muhimu ni kuhakikisha jamii inapata taarifa za kweli”alisema Yildirim

Türkei Binali Yildirim Rede
Waziri mkuu wa Uturuki Binali YildirimPicha: Getty Images/AFP/A. Altana

Uturuki inakichukulia chama cha Democratic Union cha wapigaji wa kukurdi kuwa cha kigaidi na swala hilo pamoja na lile tete kuhusu mhubiri maarufu wa kiislamu anayeishi Marekani Fethullah Gulen, ni baadhi masuala yatakayotawala mazungumzo kati ya Uturuki na makamu wa rais wa Marekani Joe Biden anayetazamiwa nchini humo hapo kesho. Gullen analaumiwa na serikali ya Uturuki kwa jaribio liloshindwa la mapinduzi ya kijeshi nchini humo tarehe 15 mwezi Julai mwaka huu

Mwandishi:Jane Nyingi/AFPE/AP

Mhariri:Daniel Gakuba