1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makamishna wepya wa Umoja wa Ulaya wachaguliwa leo

9 Februari 2010

Kukubaliwa leo na bunge la Ulaya kwa makamishna wepya wa Tume ya Ulaya kumemfanya Rais wa tume hiyo, Manuel Barroso, akubaliane na baadhi ya mambo.

https://p.dw.com/p/Lwnt
Jengo la Bunge la Ulaya mjini StrassbourgPicha: EU

Zaidi ya miezi mitatu baada ya vile ilivopangwa mwanzoni, leo makamishna wepya wa tume mpya ya Ulaya wataanza kazi zao pale kibali kitakapotolewa leo na bunge la Ulaya.

Imechukuwa wakati mrefu hadi hali hii ya sasa kufikiwa, kwa vile mtetezi wa ukamishna kutoka Bulgaria, Bibi Schelewa, alikataliwa na bunge pale alipohojiwa. Rais wa Tume ya Ulaya, Manuel Barrosa, ilimbidi atafute mtu mbadala kwa nafasi yake. Hii leo wabunge wa Ulaya kutoka kambi za Wa-Conservative, Wa-Social Democratic na Waliberali watapiga kura. Wao watatosha kuwapitisha makamishna wepya. Lakini wabunge wa vyama vya Kijani wanampiga Bwana Manuel Barroso. Mbunge Rebecca Harms:

" Fikra yangu ni kwamba Bwana Barroso si mtu barabara wa kuzipa umuhimu mpya siasa za Umoja wa Ulaya katika enzi hii ya baada ya Mkataba wa Lisbon; maisha alikuwa mtu anayesikiliza zaidi maoni ya tume na sio ya bunge la Ulaya, nami simuamini kwamba ataimarisha kuweko demokrasia, uwazi, na tume kuwa karibu na wananchi."

Pia makamishna wanaoacha madaraka wanalalamika kwamba uongozi wa Manuel Barroso ni wa kutaka lifanyike lile tu analotaka, na kwamba anataka mamlaka yawe yote mikononi mwake. Jopo la makamishna mara chache liliamua kwa sauti moja. Pia bungeni kuna kauli nyingi ambazo zinasema kwamba Bwana Barosso ni mtu wa baraza la wakuu wa nchi wanachama katika Umoja wa Ulaya.

Mbunge wa Ulaya kutoka Chama cha Christian Democratic, Werner Langen:

"Ukweli wa mambo ni kwamba pale mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya unapoamua jambo, basi tume, katika siku inayofuata, inatekeleza uamuzi huo, lakini pale bunge linapoamua jambo, basi hapo linadharauliwa."

Na ili kuibadilisha hali hiyo, ndio maana wabunge wa kutoka makundi yote ya vyama wamefikia maafikiano na Bwana Barroso, nayo ni kwamba bunge linatoa kibali chake kwa makamishna wepya wa bunge, lakini bunge hilo linapatiwa uwezo zaidi. Maafikiano ya kitaasisi, ndio jina la hati ya mapatano hayo ambayo kwamba wabunge watakuwa na ushawishi zaidi na uwezo wa kudhibiti mambo. Kutoka sasa bunge litaweza kuitaka tume ya Ulaya kuyapitia upya mapendekezo ya sheria zinazotaka kuwasilishwa bungeni; hali hii ilikuwepo hapo kabla, lakini tume ilikuwa hailazimiki kujibu. Sasa tume itabidi mnamo miezi mitatu iarifu kama inalifanyia marekebisho pendekezo ama sivyo. Pia wabunge wanataka kuziona hati zote ambazo pia wakuu wa nchi na serikali inabidi wazione. Wahakiki wanasema kwamba haki hizi mpya zina mamlaka ndani yake, kwani mkataba wa Lisbon, kwa mfano, haujafikiria jambo hili.

Mbunge Rebecca Harms anatetea hali hiyo kwa kusema kwamba wabunge mbele ya raia wanahisi wanawajibika kuunda hali nzuri za kufanya kazi ndani ya tume ya umoja wa Ulaya; na jambo hilo linahusiana na haki ya raia wa nchi za Umoja wa Ulaya kutekelezwa kwa kiwango cha juu kabisa.

Hata hivyo, kutoaminiana baina ya Bunge na Tume ya Umoja wa Ulaya kungaliko bado. Na hali hii itaonekana leo. Kwanza Manuel Barosso itambidi atoe ridhaa mbele ya bunge na aahidi kwamba yeye atawapa wabunge haki zaidi, na baada ya hapo ndipo wabunge wataamua kwamba wanataka kushauriana na tume mpya juu ya mapatano hayo, na mwisho kabisa ndipo kura zitapigwa kuwakubali makamishna wepya wa tume ya Ulaya.

Mwandishi: Christoph Prössi/Miraji Othman/ZR

Mpitiaji: Mohamed Abdulrahman