1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MAKKAH: Viongozi wa Hamas na Fatah waalikwa kwa mazungumzo

29 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCWm

Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia amewaalika viongozi wa vyama vya Hamas na Fatah nchini Palestina kwa mazungumzo mjini Mecca huku mapigano yakiendelea katika Ukanda wa Gaza.

Kiongozi wa chama tawala cha Hamas aliye uhamishoni, Khaled Meshaal na kiongozi wa chama cha Fatah, rais Mahmoud Abbas, wamesema wako tayari kuhudhuria mazungumzo ya aina hiyo, lakini tarehe ya mkutano huo haijatangazwa.

Jana watu watano waliuwawa wakati wa mapigano makali mjini Gaza, mmoja akiwa mpiganaji wa chama cha Hamas aliyeuwawa karibu na jengo la bunge.

Wapiganaji wa chama cha Hamas pia walikusanyika katika ngome ya chama cha Fatah, makao makuu ya kikosi cha kuzuia machafuko, wakitishia kukishambulia.

Msemaji wa serikali ya Hamas Ghazi Hamad amesema wanazungumza na viongozi wa Fatah kumaliza mapigano.

´Siku zilizopita tumekuwa na mawasiliano na sehemu mbalimbali za Hamas na Fatah na kamati kuu ya kitaifa ya kiislamu ya ndugu wa Misri na tunajaribu kuzuia machafuko haya yote katika barabara na kukomesha umwagikaji damu.´

Tangu Alhamisi wiki iliyopita, madaktari wanasema wapalestina 28 wameuwawa na wengine takriban 75 kujeruhiwa katika mapigano baina ya Fatah na Hamas nchini Palestina.