1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makombora ya Isreal yauwa wapiganaji 23 Syria

Sudi Mnette
10 Mei 2018

Makombra ya Israel yenye lengo la kulipiza kisasi dhidi ya Iran katika ardhi ya Syria yamesababisha vifo vya watu 23 na wengine kadhaa wamejeruhiwa.

https://p.dw.com/p/2xTzI
Syrien Raketen über Damaskus
Makombora ya Syria yanaonekana katika anga la jiji la DamascusPicha: picture-alliance/AP Photo/Syrian Central Military Media

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametoa wito wa kudhibitiwa hali ya kuendelea kwa uhasama zaidi kati ya Israel na Iran, baada ya jeshi la Israel kusema limeshambulia maeneo ya kijeshi ya Iran nchini Syria, kutokana na kile ilichokitaja kuwa kujibu mashambulizi ya roketi dhidi ya wanajeshi wake yaliofanywa na Iran. Takribani wapiganaji 23 wanaelezwa kuuawa katika mashambulizi hayo ya Israel. 

"Anatoa wito wa kudhibiti uhasama", ni maneno yaliyo katika taarifa ya rais, ikiongeza kuwa Macron atajadili suala hilo na  Kansela Angela Merkel wa Ujerumani pale watakapokutana mjini Aachen, huko magharibi mwa Ujerumani baadae leo. Jeshi la Israel limesema limeyashambulia maeneo kadhaa ya kijeshi ya Iran katika maeneo tofauti ya Syria, katika kile kinacoelezwa kuwa ni moja kati ya opereshani zake kubwa za kijeshi katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Wapiganaji 23 wameuwawa

Israelische Panzer auf den Golanhöhen
Kifaru cha Israel kikiwa katika tahadhariPicha: Getty Images/AFP/J. Marey

Waziri wa Ulinzi wa Israel Avigdor Lieberman anaelezea zaidi "Iran ndio iliyaonza kuliingilia taifa la Israel, inajaribu kufanya makabiliano dhidi yetu, na hatutaruhusu Iran iifanye Syria kuwa eneo la mashambulizi dhidi ya Israel. Hii ni sera, ni sera iliyo wazi, ni sera iliyo wazi sana, sana na tunachokitekeleza kinazingatia sera hiyo."

Israel ilifanya operesheni hiyo baada ya kusema kuwa wameshambuliwa na maroketi takribani  20 katika eneo wanalolikalia la milima ya Golan, ambapo mashambulizi hayo yalitokea upande wa Syria. Kwa mujibu wa shirika la uangalizi wa haki za binaadamu la Syria lenye makazi yake London, Uingereza operesheni hiyo imesabisha vifo vya wapiganaji 23 wakiwemo wanajeshi watano wa jeshi la Syria na wengine 18 kutoka makundi washirika.

Ujerumani yailani Iran kwa uchokozi

Kufuatia hali hiyo Ujerumani imeituhumu Iran kwa uchokozi. Katika taarifa yake msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema inalaani vikali, kama wanavyosisitiza siku zote kuwa Israel inayo haki ya kujilinda. Hata hivyo imeongeza ni muhimu kuzuwia machafuko zaidi.

Kwa upande wao Urusi, taifa mshirika wa utawala wa Rais Bashir al Assad limesema Syria ilifanikiwa kuzuwia zaidi ya nusu ya makombora ya Israel ya leo hii. Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Urusi imesema zaidi ya nusu ya makombora hayo yaliyovurumisha usiku kucha wa kuamkia leo hayakuweza kufua dafu.

Awali jeshi la Iran nchini Syria lilifyatua maroketi kwa kuelekeza katika maeneo ya kambi za Israel katika milima ya Golan, jambo ambalo Israel inasema lina lengo la kunyong'onyesha moja ya meeneo yenye nguvu kubwa kabisa ya kijeshi ya Israel dhidi ya Syria tangu mgogogoro wa taifa hilo ulipoanza mwaka 2011.

Tukio hilo linatokea baada ya wiki kadhaa za wasiwasi na kufuatia hatua ya rais wa Marekani, Donald Trump kujiondoa katika makubaliano muhimu ya mpango wa nyuklia wa Iran ya mwaka 2015, hatua ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikipigiwa chapuo na Israel. Katika mahojiano yake na gazeti la kila wiki la Der Spiegel, ambayo yalichapishwa mwishoni mwa juma lililopita Macron alisema kujiondoa kwa Marekani katika mpango huo kunaweza kusababisha vita.

Mwandishi: Sudi Mnette/AFP
Mhariri:Iddi Ssessanga