1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano kamili kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran bado

Admin.WagnerD5 Machi 2015

Marekani imesema changamoto kubwa bado zinasalia kufikia makubaliano kamili kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran lakini imeapa kutotetetereshwa katika azma yake ya kuizuia Iran kutengeza silaha za nyuklia

https://p.dw.com/p/1ElH5
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Iran Javad Zarif wamemaliza mazungumzo ya kina ya siku tatu yaliyokuwa yakifanyika nchini Uswisi tangu Jumatatu bila ya makubaliano kamili huku muda wa mwisho wa kufikiwa makubaliano kamili ambao ni tarehe 31 mwezi huu ukikaribia.

Kerry amewaambia waandishi wa habari kuwa wamepiga hatua kadhaa katika duru hiyo ya mazungumzo iliyokamilika hapo jana, lakini bado maaamuzi muhimu yanatarajiwa kuchukuliwa.

Changamoto bado zipo

Kwa upande wake Zarif alikuwa na matumaini kuwa licha ya tofauti zilizopo kati ya Iran na Marekani kuhusu mpango huo wa kinyuklia, makubaliano kamili yanaweza kufikiwa. Hata hivyo Zarif ameonya kuwa suala tete la kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Iran ambalo nchi hiyo inalenga kufikiwa huenda likatatiza kupatikana kwa makubaliano kamili iwapo halitashughulikiwa ipasavyo.

John Kerry na Javad Zarif mjini Montreaux kwa mazungumzo
John Kerry na Javad Zarif mjini Montreaux kwa mazungumzoPicha: Reuters/E. Vucci

Akizungumza siku moja baada ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuyaponda makubaliano yanayotafutwa kati ya nchi zenye nguvu zaidi duniani na Iran, Kerry amesisitiza kuwa lengo la mazungumzo ni kupatikana kwa makubaliano sahihi yanayoweza kudumu.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani ameonya kuwa nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani zinazofanya mazungumzo na Iran hazitakubali kutatizwa na ushawishi au siasa kutoka nje.

Nchi zenye nguvu zaidi duniani zinataka kuizuia Iran kurutubisha madini ya Urani katika kiwanda cha kinyuklia cha Fordo na kutanua shughuli zake za kinyuklia katika kinu cha Arak.

Duru nyingine ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran inatarajiwa kufanyika tarehe 15 mwezi huu na mazungumzo mengine ya ngazi ya kisiasa ya wawakilishi wa nchi sita zilizoko katika meza ya mazungumzo yanatarajiwa kuendelea hii leo mjini Montreux huku kundi la wataalamu wa shirika la umoja wa Mataifa kuhusu nishati ya atomiki likikutana wiki ijayo.

Saudi Arabia inatiwa wasiwasi na Iran

Kerry hii leo amewasili Saudi Arabia kufanya mazungumzo na mfalme Salman kumuhakikishia kuwa makubaliano yoyote yatakayofikiwa na Iran kuhusu mpango wake wa kinyuklia yatazingatia maslahi ya Saudi Arabia na hayatakuwa kitisho kwa kanda ya Mashariki ya kati.

Mfalme wa Saudi Arabia Salman
Mfalme wa Saudi Arabia SalmanPicha: Reuters/Saudi Press Agency

Kerry anakutana pia na mawaziri wa mambo ya nje wa Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia na umoja wa falme za kiarabu nchi za kisunni ambazo zinatiwa wasiwasi na shughuli za kinyuklia za Iran na ushawishi wa utawala wa kishia wa Iran katika kanda hiyo.

Ajenda nyingine katika mkutano huo unaofanyika Riyadh ni vita vinavyoendelea dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu nchini Syria na Iraq, pamoja na msukosuko wa kisiasa nchini Yemen. Iran inashutumiwa kwa kuunga mkono utawala wa Syria, kutoa msaada kukabiliana na wanamgambo nchini Iraq na kuwaunga mkono waasi wa Houthi nchini Yemen na kulaumiwa kwa kuichochea mizozo mashariki ya Kati.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri:Gakuba Daniel