1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya awali kuhusu mradi wa Bwawa la Mto Nile

Oumilkheir Hamidou
16 Januari 2020

Maafisa wa serikali za Misri, Ethiopia na Sudan wanasema wamefikia hatua muhimu kuelekea makubaliano kuhusu mradi mkubwa wa bwawa katika mto Nile, mradi uliokuwa ukizusha mivutano tangu miaka tisa iliyopita.

https://p.dw.com/p/3WHTi
Äthiopien Addis Abeba | Diskussion Blue Nile & Renaissance-Damm | Flaggen
Picha: DW/G. Tedla

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje na maafisa wa sekta ya maji kutoka nchi hizo tatu wamekamilisha mazungumzo ya siku tatu mjini Washington pamoja na waziri wa hazina wa Marekani Steven Mnuchin na mwenyekiti wa benki kuu ya dunia Davis Malpass.

Mradi huo uliopewa jina " Bwawa kubwa la Machipuko Ethiopia" umekamilika kwa takriban asili mia 70 na unatoa matumaini ya kukidhi mahitaji makubwa ya nishati kwa wakaazi zaidi ya milioni 100 wa Ethiopia. Hata hivyo, maafisa wa Misri wanahofia mradi wa bwawa hilo usije ukapelekea kupungua kiwango cha maji yanayohitajika nchini Misri.

Taarifa ya pamoja iliyochapishwa mjini Washington haikutoa maelezo ya muda gani utahitajika kuweza kujaza bwawa hilo, imesema tu tukio hilo litafanyika hatua kwa hatua katika msmu wa mvua ambao kawaida ni kati ya Julai hadi Agosti. Mapema mwezi huu waziri wa maji na nishati wa Ethiopia, Sileshi Bekele alisema nchi yake inataka kipindi cha miaka 12 cha kujaza bwawa hilo huku Misri ikidai kipindi cha miaka 21.

Majadiliano ya wiki hii yalilengwa kubuni kanuni na muongozo wa jinsi ya kupunguza kishindo kinachoweza kusababishwa na hali ya ukame na viwango ya maji katika bwawa hilo.

"Mawaziri wanakubaliana kwamba nchi zao tatu zina jukumu la pamoja katika kusimamia matatizo ya ukame" maafisa hao wamesema katika taarifa yao.

Makubaliano timamu huenda yakatiwa saini january 28 na 29 mjini Washington

Taarifa hiyo imeongeza kusema makubaliano ya awali kuhusu shughuli za bwawa hilo hayatokamilika hadi pale nchi husika zitakapokubaliana kuhusu vifungu vyote vya mivutano. Wawakilishi wa nchi hizo tatu wanapanga kukutana tena January 28 na 29 inayokuja mjini Washington lengo likiwa kufikia makubaliano ya mwisho kuhusu namna ya kujaza na kusimamia shughuli za bwawa hilo.

Itafaa kusema hapa kwamba bwawa hilo kubwa lenye urefu wa kilomita moja nukta nane linalokenda juu mita 145 limeanza kujengwa tangu mwaka 2012 na Etrhiopia. Mradi huo mkubwa wa mabilioni ya dala unatarajiwa kuanza kutoa umeme ifikapo mwisho wa mwaka huu wa 2020 na kukamilisha shughuli zake mwaka 2022. Linasifiwa kuwa bwawa kubwa kabisa barani Afrika likiwa na uwezo wa kuzalisha Megawat 6000 za umeme.