1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya kusitisha mapigano Libya yawe ya kuaminika:NATO

11 Aprili 2011

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Anders Fogh Rasmussen amesema hatua za kijeshi peke yake hazitotatua mzozo wa Libya na kwamba makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano lazima yaaminike na kuthibitishwa.

https://p.dw.com/p/10rQn
Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh RasmussenPicha: AP

Akizungumza leo mjini Brussels na waandishi habari, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Anders Fogh Rasmussen amesema kuwa azimio lolote lile katika mzozo huo lazima liwe lenye kujibu matakwa halali ya watu wa Libya kuhusu mageuzi ya kisiasa. Bwana Rasmussen alikuwa akisisitiza kuhusu azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaloidhinisha hatua za kijeshi dhidi ya Libya ambalo linataka kumalizika kabisa kwa vurugu dhidi ya raia.

Aidha, amesema kuwa NATO itaendelea kuvilenga vikosi vya Kanali Ghadhafi iwapo vitakuwa tishio kwa raia. Amesema operesheni ya kimataifa ya jumuiya hiyo itategemeana na lengo la wazi la kuwalinda raia dhidi ya shambulio lolote lile. NATO ilichukua rasmi jukumu kamili la operesheni za kimataifa za kijeshi nchini Libya, Machi 31 mwaka huu na katika siku za hivi karibuni imekuwa ikikosolewa na waasi wa Libya kwa kukosa ufanisi na kufanya mashambulio ya anga ambayo kwa bahati mbaya yaliwaua wapiganaji wa vikosi vya waasi.

Libyen Gaddafi Treffen Afrikanische Union NO FLASH
Ujumbe wa Umoja wa Afrika ukiwa pamoja na Kanali Muammar Gadhafi, Tripoli, LibyaPicha: AP

Kwa upande mwingine ujumbe wa Umoja wa Afrika ukiongozwa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini mapema leo ulisema kuwa Kanali Gadhafi amekubali mpango wa amani, ikiwemo kusitisha mapigano. Taarifa hizo wamezitoa baada ya kukutana na kiongozi huyo mjini Tripoli.

Hata hivyo, msemaji wa waasi kwenye mji wa Benghazi amesema upinzani utauangalia mpango huo, lakini Kanali Gadhafi lazima aondoke madarakani. Ujumbe huo wa Umoja wa Afrika ulikwenda Benghazi kukutana na viongozi wa waasi leo lakini ulipokelewa na zaidi ya waandamanaji 2,000 waliokuwa wamebeba mabango yaliyoandikwa ujumbe unaosema, ''Umoja wa Afrika mchukueni Ghadhafi pamoja nanyi na Gadhafi amefanya mauaji ya halaiki.''

Libyen Soldaten und Plakat von Muammar Gaddafi in Tripolis
Wanajeshi wanaomtii Kanali GadhafiPicha: dapd

Wakati huo huo, vikosi vinavyomtii Kanali Gadhafi leo vimeshambulia mji wa Misrata, muda mfupi baada ya Umoja wa Afrika kusema kuwa kiongozi huyo amekubali mpango wa kusitisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Kituo cha televisheni cha Al-Jazeera kilimnukuu msemaji wa waasi akisema kuwa watu watano wameuawa na wengine 20 wamejeruhiwa huko Misrata, eneo pekee la waasi lililoko magharibi mwa Libya ambalo limekuwa likizingirwa kwa zaidi ya wiki sita sasa. Waasi wa Misrata wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa vikosi vya Kanali Gadhafi vilirusha maroketi yaliyotengenezwa nchini Urusi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE,APE)
Mhariri:Josephat Charo