1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya kusitisha mapigano Syria hatarini

Mohammed Khelef18 Septemba 2016

Usitishaji mapigano nchini Syria uko hatarini kuvunjika, huku Urusi na Marekani zikishutumiana kwenye katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia kikao cha dharura kujadili mashambulizi ya Marekani.

https://p.dw.com/p/1K4La
Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Samantha Power (aliyesimama kulia), akitupiana maneno na mwenzake wa Urusi, Vitaly Churkin (aliyekaa).
Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Samantha Power (aliyesimama kulia), akitupiana maneno na mwenzake wa Urusi, Vitaly Churkin (aliyekaa).Picha: picture-alliance/dpa/J. Szenes

Urusi ilikasirishwa na kitendo cha Marekani kukiita kikao hicho cha dharura kuwa ni cha "mazingaombwe." Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin, alitoka nje ya kikao hicho kwa hasira, akimtuhumu mwenzake wa Marekani, Samantha Power, kwa kutumia lugha isiyo heshima.

"Siwajawahi kushuhudia kiwango kikubwa cha ubadilishaji kauli cha Wamarekani kama tulivyoshuhudia leo," alisema Balozi Churkin baada ya kutoka kwenye mkutano huo ambao nchi yake uliutisha.

Churkin alisema Power alimuambia hakuwa na hamu ya kukisikiliza kile ambacho yeye (Churkin) alikuwa anataka kukisema kwa sababu mkutano huo ulikuwa ni "mazingaombwe", kauli ambayo ilimfanya Churkin kutoka kikaoni.

"Jambo hili ni kubwa sana ambalo tulitaka kushirikiana taarifa zake na Baraza la Usalama. Ni jambo la kutia wasiwasi sana kwamba Marekani ilichaguwa kufanya mashambulizi ya anga Syria katika wakati kama huu," alisema Churkin baada ya kutoka kwenye mkutano huo.

Katika kikao hicho cha ndani, Balozi Power alisema Urusi inajionesha ilivyo kigeugeu, akiongeza kuwa "hata kwa vigezo vya Urusi, mazingaombwe ya usiku huu - mazingaombwe yaliyofichwa nyuma ya maadili na misimamo - ni ya unafiki wa kipekee."

Balozi huyo wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa alisema Urusi haijawahi kuitisha kikao cha dharura pale jeshi la Syria linapovishambulia vikosi vya waasi au kuzuia misaada isifike maeneo linayoyazingira. "Sasa kwa nini tunafanya mkutano huu usiku huu? Ni namna ya kujibereuza kwa kile kinachotokea kwenye Syria hivi sasa," alisema Power.

Taarifa za awali zinasema kuwa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani umekiri kuwa huenda umevishambulia vituo vya jeshi la Syria kaskazini mwa nchi hiyo, katika mashambulizi ambayo Urusi na kundi la waangalizi wanasema yaliuwa wanajeshi 62 wa serikali.

Makubaliano ya kusitisha mapigano mashakani

Mashambulizi hayo yalifanyika ikiwa ni chini ya wiki moja tangu kuanza kwa usitishaji mapigano unaolegalega, uliokuwa umekusudiwa kuzuia umwagaji damu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea kwa mwaka wa tano nchini Syria, huku Urusi ikiwatuhumu wale wanaoitwa "waasi wenye msimamo wa wastani" kwa kusababisha kushindwa kwa makubaliano hayo.

Waokoaji wakisaka watu kwenye kifusi cha jengo baada ya mashambulizi yanayoshukiwa kufanywa na Marekani kusini mashariki mwa Syria.
Waokoaji wakisaka watu kwenye kifusi cha jengo baada ya mashambulizi yanayoshukiwa kufanywa na Marekani kusini mashariki mwa Syria.Picha: Getty Images/AFP/T. Mohammed

Maafisa wa Marekani walisema kuwa muungano huo wa kijeshi unaopambana na magaidi wa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS) nchini Syria huenda waliyapiga maeneo ya jeshi la serikali. "Vikosi vya majeshi washirika viliamini vinashambulia eneo la Daa'ish," ilisema taarifa ya makao makuu ya jeshi la Marekani, Pentagon, ikilitaja kundi la IS kwa jina lake la Kiarabu (Daa'ish).

Lakini taarifa hiyo ikaendelea kusema kuwa mashambulizi hayo yalisitishwa haraka, mara tu maafisa wa muungano huo wa kijeshi walipotaarifiwa na wenzao wa Urusi kwamba "kulikuwa na uwezekano magari yaliyolengwa yalikuwa ni sehemu ya kikosi cha jeshi la Syria."

Wakati ikiitisha kikao hicho cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Urusi ilisema inataka serikali ya Marekani itowe taarifa ya kina na kamili mbele ya Baraza hilo. Jeshi la Urusi linadai kuwa endapo makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza kutekelezwa Jumatatu iliyopita (12 Septemba) yatavunjika, ni Marekani inayostahiki lawama.

Likithibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo, Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake London, Uingereza, linasema idadi ya wanajeshi wa serikali waliouawa ni 83, ingawa taarifa ya jeshi la Urusi ilisema wanajeshi waliouawa ni 64 katika eneo la Deir Ezzor, ambalo limezijngirwa na wapiganaji wa IS.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa, AFP
Mhariri: Isaac Gamba