1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali yajitayarisha kwa vita; Majirani wana shaka

29 Septemba 2012

Viongozi wa Mali wanajitayarisha na vita, kulikomboa eneo la kaskazini linalodhibitiwa na makundi ya waasi wa Kiislamu: ni ujumbe kutoka Bamako katika mkutano wa umoja wa mataifa,licha ya majirani zake kuwa na shaka.

https://p.dw.com/p/16HMJ
Modibo Diarra waziri mkuu wa MaliPicha: Reuters

Tunahisi kuwa jumuiya ya kimataifa inawajibika kwa upande wetu, ikiwa ni mshikamano na Mali, duru karibu na rais Dioncounda Traore ililiambia shirika la habari la AFP.

Alikuwa akizungumza katika mkutano siku ya Jumatano mjini New York, pembezoni mwa mkutano wa hadhara kuu ya umoja wa mataifa, ambao ulikuwa unalenga kujadili kuhusu mzozo wa eneo la Sahel.

Maafisa wa Mali wanatambua kuwa majirani wa nchi hiyo Algeria inajaribu kuleta hali ya maelewano na Mauritania na Niger ili kuzuwia uwekaji wa majeshi ya kigeni nchini Mali, kimesema chanzo hicho.

Mali militante Bewegung MUJWA
Kundi la waasi wa Kiislamu nchini Mali la MUJWAPicha: Reuters

Lakini Ufaransa itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa baraza la usalama linakutana na azimio linaloidhinisha kuingilia kati linapatikana, ameongeza afisa huyo.

Raia wanaunga mkono

Mjini Bamako , "watu hawaulizi tena lini vita vitaanza ?, lakini vipi tunaweza kuweka pamoja masharti muhimu ya kuanzisha vita. Kwetu sisi, uingiliaji kati hauko mbali sana, unatayarishwa, chanzo hicho kimeeleza. Madou Diallo, profesa wa sheria za kimataifa katika chuo kikuu cha mjini Bamako, jibu kutoka kwa jumuiya ya kimataifa limepunguka makali na la kujizuwia zaidi.

Tunafahamu mapendekezo ya kuchukua tahadhari ya hali ya juu , kwa upande wa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon, kwasababu vita hivi vinaweza kusababisha maafa ya kiutu, Diallo amesema.

Krise im Norden von Mali Flüchtlinge in Burkina Faso
Mzozo wa Mali umesababisha mzozo wa wakimbiziPicha: picture-alliance/dpa

Lakini wananchi wa Mali kwa jumla inapendelea hatua ya kuingilia kati upande wa kaskazini, ameongeza. "Hicho ndio kinasikika mitaani".

Magazeti yako upande gani?

Magazeti nchini Mali hata hivyo yalijishughulisha na masuala mengine.

Hawakutoa umuhimu katika vichwa vya habari katika mjadala unaoendelea katika umoja wa mataifa lakini wameelekeza kalamu zao katika mapambano nchini Mali baina ya makundi hasimu ya jeshi la polisi ambapo watu wawili wamejeruhiwa.

Ghasia kama hizo ni matokeo ya hali ya wasi wasi ambayo imekuwapo kwa miezi kadha baada ya mapinduzi ya mwezi Machi ambayo yamemwondoa madarakani rais Amadou Toumani Toure, ambaye amekuwa madarakani kwa muda wa miaka kumi.

Dioncounda Traore Mali Präsident
Rais wa Mali Dioncounda TraorePicha: AP

Jeshi na wanasiasa wanavutana

Mjini Bamako kuna hali ya wasi wasi sana kati ya wanasiasa na jeshi, amedokeza Gille Yabi, mwakilishi wa Senegal katika kundi la uchunguzi wa mizozo la kimataifa, ICG.

Jeshi la Mali ni jeshi la baada ya mapinduzi na linahitaji kutambuliwa na kupewa jukumu katika mapinduzi hayo, ambapo linawakilisha ukoo muhimu ndani ya jeshi hilo.

Mazungumzo yamepangwa kufanyika mwezi Oktoba katika mji mkuu wa Mali, Bamako, ambako wahusika wote, vyama vya siasa, vyama vya kijamii, makundi ya kidini na jeshi , wanaweza kufikia makubaliano juu ya vipi kipindi cha mpito cha kisiasa kinaweza kushughulikiwa, kimesema chanzo hicho cha habari kutoka ofisi ya rais.

Uundwaji wa baraza kuu la taifa umeahirishwa, likiwa na makamu wawili wa rais, mmoja akiwa na jukumu la ulinzi.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Bruce Amani