1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malkia Elizabeth II wa Uingereza atimiza miaka 92

Daniel Gakuba
21 Aprili 2018

Sherehe kubwa zinafanyika katika kasli la kifalme mjini London, Uingereza, kuadhimisha miaka 92 ya kuzaliwa Malkia wa nchi hiyo, Elizabeth II. Sharehe hizo zimekwenda sambamba na mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Madola.

https://p.dw.com/p/2wRku
Queen Elizabeth II
Picha: Getty Images/AFP/A. Grant

Malkia wa Uingereza, Elizabeth II amesherehekea miaka 92 ya kuzaliwa, katika sherehe iliyohudhuriwa na nyota kadhaa katika fani ya burudani. Mizinga ya kukokotwa na farasi imefyatuliwa mara 41 kwa heshima yake katika bustani ya Hyder Park na mara 61 kwenye mnara wa London. Kwenye Kasli la Windsor, kikosi cha ulinzi wa ufalme kimemwimbia Malkia Elizabeth II wimbo wa ''Happy Birthday'' wakati wa kubadilishana zamu.

Jioni ya leo Malkia na familia yake wanatarajia kutumbuizwa na wasanii kutoka nchi mbali mbali za Jumuiya ya Madola. Wakuu wa jumuiya hiyo yenye nchi 53 wanachama wamekuwa wakikutana mjini London katika mkutano wao wa kilele unaofanyika kila baada ya miaka miwili.

Wasanii watakaotumbuiza hafla hiyo  ni pamoja na Kylie kutoka Australia, Shawn Mendes kutoka Canada, bendi ya Ladysmith Black Mambazo ya Afrika Kusini, na nyota wa Reggae Mmarekani mwenye asili ya Jamaica, Shaggy. Kutoka Uingereza kwenyewe wasanii watakaoshiriki katika sherehe hiyo ni Tom Jones, Craig David na Sting.

Katika sherehe hizo zitakusanywa fedha zitakazowekwa katika fuko la hisani la Malkia Elizabeth, ambalo linasimamiwa na mjukuu wake, Mwanamfalme Harry ambaye pia anatarajiwa kutoa hotuba.

Malkia Elizabeth II amekuwa kama nembo ya Jumuiya ya Madola inayoishirikisha Uingereza na nchi zilizowahi kuwa makoloni yake, tangu kufariki kwa baba yake, Mfalme George VI mwaka 1952.