1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mambo bado ni moto kati ya Obama na Clinton.

7 Mei 2008

Barack Obama ashinda kiulaini huko Carolina ya Kaskazini wakati Hilary Clinton ashinda kwa taabu huko Indiana katika chaguzi za kuwania tiketi ya urais kupitia chama cha Demokrat.

https://p.dw.com/p/Dv25
Hawa ndio wanaowania kuteuliwa na vyama vyao kugombania urais wa Marekani.John McCain anawania na chama tawala cha Republican wakati Hillary Clinton na Barack Obama wanawania kupitia chama cha Demokrat.Picha: AP GraphicsBank

Barack Obama amepiga hatua kubwa katika chaguzi za awali kuwania uteuzi wa rais kupitia chama cha Demokratik nchini Marekani kwa ushindi laini huko Carolina Kaskazini hapo jana na Hilary Clinton ameapa kuendelea kuipa nguvu kampeni yake baada ya kushinda chupu chupu huko Indiana.

Matokeo ya jana yamemsaidia Obama kuzidi kutanuwa katika kuongoza dhidi ya Clinton katika mchuano mkali wa kugombea tiketi ya kuwania urais kupitia chama cha Demokratik na hiyo kuja kupambana na John McCain mgombea wa chama tawala cha Republican katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika nchini Marekani hapo mwezi wa Novemba huku kukiwa kumebakia chaguzi sita tu za kuwania uteuzi huo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara kushehereka ushindi huko Raleigh Carolina ya Kaskazini Obama amesema wameona kwamba ni jambo linalowezekana kuondokana na siasa za utengano na kupotosha malengo kwamba ni jambo linalowezekana kuachana na kushambuliana vibaya kwa nia tu ya kujishindia hoja na si kamwe juu ya kutatuwa matatizo yao.

Obama mwenye umri wa miaka 46 ameonekana kama alikuwa tayari amejiandaa kwa mpambano wa kuwania urais na John McCain katika uchaguzi mkuu.Obama iwapo atashinda atakuwa rais wa kwanza mweusi wa Marekani amesema katika kipindi hiki wanakusudia kusonga mbele kama chama kimoja cha Demokratik kilichounganishwa na mtizamo mmoja kwa nchi hiyo kwa sababu wote wanakubaliana na hilo katika wakati huu muhimu katika historia yao.

Obama anasema wakati ambapo wanakabiliana na vita viwili ...uchumi ukiwa kwenye machafuko na dunia ikiwa katika hatari, matumaini ambayo kwayo inaonekana kuwaponyoka Wamarekani wengi.Amesema hawamudu kumpa nafasi John McCain kutumikia kipindi cha tatu cha utawala wa Bush kwamba wanahitaji mabadiliko nchini Marekani na ndio sababu watakuwa wameungana hapo mwezi wa Novemba

.

Ushindi wa asilimia 14 wa seneta huyo wa Illinois huko Carolina ya Kaskazini ilikuwa ni kurudi kutamba kwa vishindo kutoka katika kampeni ngumu ilioanza mwezi uliopita na kushindwa vibaya huko Penyslvania na kurefushwa na utata kutokana na matamshi ya kibaguzi yaliotolewa na kasisi wake wa zamani Mchungaji Jeremeiah Wright.

Matokeo hayo yanaamanisha kwamba Hilary Clinton amepoteza fursa nzuri kabisa ya kupunguza pengo la kuongoza kwa Obama katika ahadi za wajumbe ambao watasaidia kumchaguwa mgombea katika mkutano mkuu wa chama cha Demokratik hapo mnwezi wa Augusti.

Clinton ameshinda Indiana kwa kura 23,000 tu kutoka zaidi ya kura milioni moja nukta 25 zilizopigwa katika jimbo hilo lakini ameahidi kuendelea na mapambano.

Amesema wamechomoka kutoka nyuma na kusonga mbele kutokana na wananchi na sasa kasi ni moja kuelekea Ikulu.

Clinton mwenye umri wa miaka 60 seneta wa New York na mama rais wa zamani ambaye akishinda atakuwa rais wa kwanza mwanamke nchini Marekani ameutaka umati wa Indianapolis ambao alikuwa akiuhutubia kutowa michango kuipa uhai kampeni yake ambayo kwa matumizi imezidiwa na ile ya Obama.

Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuzorota kwa uchumi wa Marekani ambako kumezidi kuwashughulisha wapiga kura nchini kote lilikuwa ni suala kuu kwa theluthi mbili ya wapiga kura wa Indiana na asilimia sita kwa wapiga kura wa Carolina ya Kaskazini.