1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamia wazama baharini wakielekea Ulaya

Admin.WagnerD3 Juni 2016

Mamia ya wakimbizi wanahofiwa kuwa wamekufa maji baada ya boti yao kupinduka na kuzama kusini mwa kisiwa cha Ugiriki cha Crete. Watu mia saba walikuwamo ndani ya boti hiyo.

https://p.dw.com/p/1J0BO
Wakimbizi waliokolewa katika kisiwa cha Crete
Wakimbizi waliokolewa katika kisiwa cha CretePicha: Getty Images/AFP/STR

Taarifa ya shirika hilo imesema watu 250 waliweza kuokolewa.

Msemaji wa walinzi wa pwani ya Ugiriki Nikolaos Lanadianos ameliambia shirika la televisheni la serikali kwamba watu hao waliokolewa na kwamba juhudi za kuwatafuta watu wengine zinaendelea.

Huenda idadi ya vifo ikaongezeka

Vyombo vya habari vya nchini Ugiriki vimeripoti kuwa maiti nyingi zimeopolewa kutoka baharini. Msemaji wa shirika la kimataifa la kuwahudua wahamiaji IOM, Joel Millman amethibitisha juu ya kuokolewa watu hao na amesma kuwa juhudi za kuwatafuta watu wengine zinaendelea.

Msemaji huyo ameeleza kuwa huenda idadi ya watakaokufa ikaongezeka kwa kadri siku inavyosonga mbele.

Walinzi wa pwani ya Ugiriki wamesema chombo cha baharini kilichokuwa na urefu wa mita 25 kilichofanana na boti ya kuvulia samaki kilikuwa kinawasafirisha mamia ya wakimbizi, kilipoonekana kusini ya kisiwa cha Crete. Nusu ya boti hiyo ilikuwa imezama wakati ilipoonekana.

Boti hiyo ilianza safari yake katika mji wa Alexandria nchini Misiri.

Msemaji wa shirika la kimataifa linalowashughulikia wahamiaji bwana Millman ameeleza kuwa kisiwa cha Crete cha nchini Ugiriki kimegeuka kuwa kituo kipya cha wahamiaji na wakimbizi. Amearifu kwamba katika siku tatu zilizopita idadi ya wakimbizi wanaokusanyika kwenye kisiwa hicho imekuwa inaongezeka .

Bwana Millman amefahamisha kwamba idadi kubwa ya wakimbizi hao, wanaopitia katika njia hiyo mpya wanatoka Afghanistan,Syria na Iraq.

Njia mpya yagunduliwa na matapeli

Kutokana na njia ya Balkan,yaani kusini mwa Ulaya ,kufungwa mnamo mwezi wa Machi, iliyokuwa lango kuu la kuingilia barani Ulaya, lililotumiwa na wakimbizi mwaka uliopita, wasafirishaji haramu sasa wanaitumia njia ya Misri na kupitia kwenye kisiwa cha Crete ili kufika Italia . Katika siku za hivi karibuni wahamiaji 180 walitia nanga kwenye kisiwa hicho baada ya chombo chao kufikwa na matatizo baharini.

Juhudi za kuwaokoa wakimbizi zaendelea
Juhudi za kuwaokoa wakimbizi zaendeleaPicha: picture-alliance/AP Photo/P. Giannakouris

Kwa mujibu wa shirika la kimataifa linalowashughulikia wakimbizi, IOM wahamiaji wapatao 47,000 walivuka bahari ya Mediterania na kufika Italia katika kipindi cha miezi mitano iliyopita mnamo mwaka huu. Na 2061 kati ya hao walikufa baharini. Maafa ya leo ni ya pili kutokea kwenye bahari ya Aegean, katika kipindi kifupi cha wiki moja.

Mwandishi:Mtullya abdu/DW,afpe,dpa,

Mhariri:Iddi Ssessanga