Manchester City yaipiku Liverpool ubingwa wa Premier League
13 Mei 2019Manchester City walilazimika kupambana hadi dakika ya mwisho baada ya kuburuzwa na Liverpool lakini walipata njia na kurejea ushindi wao kama machampioni nchini humo. Timu iliyoshangaza ni Wolves, pia kuondoka kwa kocha nyota Mourinho na bila shaka ni mshangao na masikitiko makubwa, ni baadhi ya matukio mengine katika msimu huu.
Vuta nikuvute kati ya Manchester City na Liverpool itatambulika milele kuwa ni mpambano mkali wa kuwania ubingwa nchini England.
Mvutano baina ya Manchester City na Liverpool ambapo hakuna timu iliyotaka kupoteza ulikwenda hadi katika siku ya mwisho ya mchezo wa msimu na pale vumbi lilipotulia ilikuwa ni Pep Guardiola wa Manchester City ndie aliyenyakua taji hilo kwa mara ya pili kwa mwaka wa pili mfululizo. Na katika mkutano na waandishi habari Pep Guardiola alisema.
"Ubingwa mfululizo ni mgumu sana, kwa hiyo kwa msimu wa kwanza ulikuwa barabara kabisa, lakini msimu huu tulikuwa na mpinzani mgumu zaidi, kwa hiyo nawapongeza Liverpool pia kwa msimu mzuri kabisa, lakini tumefanikiwa. Tumewashinda."
Liverpool ilionekana kuwa njiani kunyakua taji hilo katika muda wa miaka 29 wakati walipokuwa na miadi na Man City Januari 3 ikiwa na nafasi ya kufungua mwanya wa pointi 10. Lakini mabingwa watetezi Man City walipambana na kupata ushindi wa mabao 2-1 na kurusha konde la kwanza katika mpambano huo wa vigogo. Ni kipigo pekee cha Liverpool katika msimu huu na kufungua mlango kwa City , kuchukua uongozi mwezi Februari. Kocha wa Liverpool Juergen Klopp aliipongeza pia Man City.
"Inakatisha tamaa , sio muda wa furaha, sio hasa hivyo, lakini tunao muda wa kutosha kupata kujua ni kitu gani na kuangalia na kuhisi pengine kuwa msimu huu ulikuwa mzuri sana. Ilikuwa safi sana, pointi 97 ni jambo bora sana, na ni kwasababu tu Manchester City ilikuwapo, basi haitoshi. Katika nchi nyingine ingekuwa rahisi na kutosha, lakini hapa, hivyo ndio ilivyo. Hakuna shida na hilo, huo ni mpambano ambao tumo , sio mashindano ya miaka ya 30, ya miaka ya 20 , ama miaka 10 iliyopita, ni tofauti kabisa na vijana hawa walikuwa tayari kupambana na nawapa heshima zangu. Sio tu wao kwasababu lazima niseme watu wengi wanasema juu ya mashabiki wa Liverpool , kwamba wanataka sana kushinda ligi, na vitu kama hivyo. Vile walivyotufuatilia, inafurahisha. Klabu hii imo katika wakati wake mzuri sana kwa muda mrefu na haitaishia hapo kwasababu kuna timu moja ina pointi moja zaidi."
Europa League
Chelsea ilimaliza ikiwa nafasi ya tatu pointi 25 nyuma ya Liverpool, lakini ilitosha kuwapa nafasi ya kucheza katika Champions League msimu ujao pamoja na Tottenham. Arsenal katika msimu wao wa kwanza na kocha Unai Emery , na Manchester United walikuwa nyuma wakipata fursa ya kucheza Europa League.
Lakini iwapo Arsenal itashinda mchezo wake wa fainali dhidi ya Chelsea katika Europa league itajiunga na timu nne za England katika Champions League msimu ujao.
Wolverhamton Wanderres ilimshangaza kila mmoja kwa kumaliza nafasi ya saba baada ya kurejea katika Premier League na pia itafuzu kucheza katika Europa League iwapo City itashinda kombe la FA Jumamosi katika fainali dhidi ya Watford, ambayo itapata nafasi hiyo iwapo itashinda.
Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amezionya timu nyingine katika Premier League kwamba mabingwa hao wataendelea kuwa bora na imara baada ya kuiweka kando Liverpool na kuwa timu ya kwanza katika muda wa muongo mmoja kunyakua mfululizo taji la Premier League.
"Hii ni ligi ngumu kabisa niliyoweza kushinda kuanzia mwanzo. Nilishinda Uhispania, nilishinda Ujerumani, lakini hii ni ligi ngumu sana, hususana ushindani tuliokabiliana nao msimu mzima."
Wakati hupo huo kocha wa Liverpool Juergen Klopp amewataak wachezaji wake kutumia maumivu ya kushindwa kwao katika Premier League kuwa ni chachu ya kumaliza msumu huu na ubingwa wa Champions League wiki mbili zijazo.
Nae kocha wa Manchester United moja kati ya timu vigogo nchini England na barani Ulaya Ole Gunnar Solskjaer amesema timu yake itachukua muda kuweza kuziba mwanya uliopo kati yake na timu za Manchester City na Liverpool baada ya kumaliza msimu huu kwa kipigo cha mabao 2-0 nyumbani na Cardiff City ambayo tayari imeshuka daraja. United imemaliza ikiwa katika nafasi ya sita , ikiwa pointi 32 nyuma ya mabingwa Manchester City.
Wachezaji watatu wamefungana katika kinyang'anyiro cha kuwania kuwa mfungaji bora wa msimu, ambapo wachezaji watatu kutoka bara la Afrika wamenyakua kiatu cha dhahabu katika kinyang'anyiro hicho. Wachezaji hao ni Sadio Mane, Pierre-Emerick Aubameyang na Mohammed Salah.