1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mandela kuzikwa Jumapili

15 Desemba 2013

Nelson Mandela atazikwa leo Jumapili(15.12.2013)katika mazishi yatakayofanyika kwa mila na utamaduni wa kabila lake na fahari ya nchi hiyo ambayo aliibadilisha wakati akiwa mpiganaji na hata wakati akiwa rais.

https://p.dw.com/p/1AZtK
Nelson Mandela Sarg African National Congress ANC Zeremonie
Jeneza lililochukua mwili wa MandelaPicha: Getty Images

Mazishi yake katika kijiji cha Qunu ambako aliishi wakati wa utotoni wake , yanafunga ukurasa wa mwisho wa maisha yake ambapo amekuwa mtu mashuhuri ambaye ujasiri wake na utu wake umemuweka kuwa alama duniani ya uhuru na matumaini.

Na mazishi hayo yanafikisha mwisho siku kumi za maombolezo ya kitaifa ambapo mamia kwa maelfu ya Waafrika kusini walijitokeza katika mvua pamoja na jua kali kuomboleza, kukumbuka na kusherehekea maisha ya rais wa kwanza mweusi kuchaguliwa kuiongoza nchi hiyo.

Nelson Mandela Sarg
Mwili wa Mandela ukiwasili QunuPicha: picture-alliance/dpa

Viongozi wa kisiasa kuhudhuria mazishi

Mazishi yanaanza saa mbili asubuhi saa za Afrika kusini kwa tukio la wazi litakalofanyika kwa muda wa saa mbili ambalo litahudhuriwa na karibu watu 4,500 waalikwa, ikiwa ni pamoja na viongozi waandamizi wa kisiasa pamoja na idadi kubwa ya watu mashuhuri kutoka mataifa ya kigeni.

Wananchi wa kawaida hawataruhusiwa kuona mazishi yenyewe , kwa kuwa familia imesisitiza kuwa yatafanyika kwa faragha pamoja na marafiki tu wa karibu. Eneo la makaburi liko katika shamba kubwa la familia ya Mandela lililoko katika kijiji cha Qunu lililojengwa mara baada ya kuachiliwa kutoka jela mwaka 1990, katika eneo lenye nyasi za kijani , na milima ya Cape ya mashariki.

Nelson Mandela Sarg African National Congress ANC Zeremonie
Shughuli ya kuuaga mwili wa Mandela ya chama cha ANCPicha: Getty Images

"Ni kijiji ambacho nilipitisha baadhi ya miaka ya furaha kubwa katika maisha yangu ya utoto na ambako naweza kukumbuka mambo ya mwanzo kabisa ," ameandika katika kitabu chake cha kumbukumbu. Watayarishaji wamesema kiasi ya watu 450 , ikiwa ni pamoja na mjane wa Mandela Graca Machel na mkewe wa zamani Winnie Madikizela-Mandela watashiriki katika mazishi ya faragha, ambayo yatafanyika kwa mujibu wa mila za kabila la Xhosa.

Yakiongozwa na wanaume wa ukoo wake, shughuli hiyo itajumuisha kuchinja ng'ombe, mila ambayo hufanywa katika muda mbali mbali wa maisha ya mtu. Katika shughuli hiyo, Mandela atajulikana kama Dalibhunga, jina alilopewa katika umri wa miaka 16 baada ya kuingia jandoni na kutiwa tohara hatua inayomuingiza mtu kuwa mtu mzima.

Mila na desturi za Xhosa

Waombolezaji watavaa mavazi ya asili ya kabila la Xhosa , yakiwa ni pamoja na kofia zenye shanga za za rangi ya kibuluu na nyeupe. Kabila la Xhosa limegawanyika katika makundi kadha, ikiwa ni pamoja na Watembu, ambao ndiko anakotokea Mandela .

Nelson Mandela Abschied 13.12.2013
Waombolezaji Wazungu kwa Waafrika wakitokwa na machoziPicha: Reuters

Licha ya kuwa Mandela hakutangaza hadharani anafuata imani ya kanisa gani , familia yake inafuata imani za kanisa la Methodist. Mipango ya mazishi iligubikwa kwa muda na malalamiko ya rafiki wa karibu wa Mandela na mshindi mwenzake wa nishani ya amani ya Nobel Desmond Tutu ambaye amesema hakualikwa kuhudhuria mazishi hayo.

Hata hivyo Jumamosi jioni Tutu alisema atahudhuria mazishi baada ya serikali kujaribu kupooza mtafaruku huo na kuuita kuwa ni kulikuwa na hali ya kutofahamiana.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / dpa

Mhariri: Bruce Amani