1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni : Fursa ya Pili kwa Tsipras

Admin.WagnerD21 Septemba 2015

Alexis Tsipras ameibuka mshindi katika uchaguzi Ugiriki hapo Jumapili. Mwandishi wa DW Spiros Moskovou anatilia mashaka iwapo kiongozi huyo ataweza kufanikisha mageuzi magumu ya kiuchumi.

https://p.dw.com/p/1GZze
Moskovou Spiros mwandishi wa Idhaa ya Ugiriki DW
Alexis Tsipras waziri mkuu wa Ugiriki kufuatia ushindi wa uchaguzi mku nchini humo.Picha: Reuters/A. Bonetti/Syriza Press Office

Hapo mwezi wa Januari Syriza ilijipatia ushindi wake wa kwanza katika uchaguzi mkuu nchini Ugiriki.Wakati huo wananchi wengi waliamini kwamba kiongozi wa chama hicho Alexis Tsipras ataweza kuipunguzia jamii taathira ya makali ya mageuzi ya kiuchumi yaliokuwa yakiendelea kutekelezwa nchini humo kwa miaka mitano iliopita.

Tsipras aliahidi kukomesha sera ya kubana matumizi. Lakini ahadi yake hiyo iliishia patupu : Baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo ilibidi akubali masharti ya wafadhili wa kimataifa kwa ajili ya kupatiwa mkopo wa tatu wa kuiepusha nchi hiyo isifilisike na madeni na kulazimika kutoka kwenye kanda inayotumia sarafu ya euro barani Ulaya.

Hivi sasa Tsipras amerudishwa tena madarakani. Wananchi wengi wa Ugiriki wamemtuza kwa kubadili msimamo kutoka ule wa kuzingatia mambo kwa fikra na kuwa ule wa kuzingatia uhalisia na kumuamini kuchukuwa jukumu la kupunguza athari kwa jamii kutokana na hatua za kufanya mageuzi zaidi ambayo yanatakiwa kutekelezwa kwa haraka.

Kitengo cha sera kali za mrengo wa kushoto kilichojitenga na chama hicho cha Syriza kupinga kukubali kwa kiongozi huyo hatua za kubana matumizi hakikuweza kupata hata asilimia tatu ya kukiwezesha kuingia bungeni.

Lakini bado ni jambo la kutiliwa mashaka iwapo Tsipras na chama chake cha Syriza wataweza kuupigisha hatua mchakato wa kuifanya nchi hiyo iwe ya kisasa.Katika kipindi cha miaka mitano iliopita Ugiriki imeshuhudia kuundwa kwa serikali tano zenye itikadi tafauti za kisiasa zikiingia na kutoka na hakuna hata moja kati yao ilioweza kufanya mabadliko ya msingi.

Moskovou Spiros mwandishi wa Idhaa ya Ugiriki DW.
Moskovou Spiros mwandishi wa Idhaa ya Ugiriki DW.

Madai ya wafadhili yamebakia pale pale : Kuanzisha sekta ya serikali inayoweza kufanya kazi kwa ufanisi, uchumi wenye ushindani na kupiga vita rushwa na ukwepaji kodi. Vyama vikubwa vinavyotabulikana tokea jadi vimeshindwa kufanikisha hayo na Syriza haikupiga hatua yoyote ya maendeleo ya maana katika miezi yake saba ya kwanza madarakani.Hatua za kwanza zilizotekekelezwa na serikali yake hiyo zilikuwa za kauili zaidi badala ya maendeleo zikitaka kuwa na taifa imara litakalomuangalia na kumgharamia kila raia.

Suala liliopo je serikali ya pili ya Tsipras itabadili mwenendo wake? Jibu haionekani hivyo!

Mara baada ya matokeo ya uchaguzi kujulikana hapo Jumapili imedhihirika kwamba mshirika wa zamani wa Syriza katika serikali ya mseto chama huru cha kizalendo cha ANRL kitamsaidia tena Tsipras kupata wingi wa viti bungeni vinavyohitajika kuunda serikali.

Katika mahojiano ya hivi karibuni Tsipras amekiri amekuja kutanabahi juu ya nguvu za fedha wakati wa mazungmzo ya kukatisha tamaa na wafadhili wa kimataifa. Hakuna matumaini makubwa ya kuwepo kwa mustakbali mwema kutokana na namna anavyotowa taarifa zake za kujijengea umaarufu wakati sera zake zikitishia maisha yenyewe ya wananchi wake.

Si jambo la kushangaza hata chembe kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya hivi karibuni mahala ilikozaliwa demokrasia aslimia 45 ya wapiga kura hakushiriki kupiga kura.

Mwandishi : Spiros Moskovou/Mohamed Dahman/

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman