1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Guaido anategemea mataifa ya nje

Mohammed Khelef
6 Machi 2019

 Kiongozi wa upinzani Juan Guaido, alirejea Venezuela akikaidi vikwazo vyote dhidi yake kutoka kwa hasimu wake, Rais Nicolas Maduro, lakini anasema Uta Thofern inavyoonekana Guaido anategemea zaidi mataifa ya kigeni.

https://p.dw.com/p/3EX7n
Venezuela l Rückkehr des Interimspräsident Guaidó
Picha: picture alliance/NurPhoto/R. B. Sierralta

Guaido hakurudi nyumbani kama alivyoondoka kwa kifichoficho akivuuka mpaka wa porini. Hapana, Guaido alitua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Caracas, akapitia madawati yote ya udhibiti wa hati za kusafiria bila kufanywa chochote na huko nje akapokelewa na wafuasi wake. Kama vile rais wa kweli.

Lakini kuwepo kwa mabalozi wa mataifa kadhaa, akiwemo wa Ujerumani, kumpokea Guaido kuliashiria kuwa urais wake wa mpito bado uko mbali sana na kuthibitishwa ndani ya nchi. Anachokihitaji zaidi ni jicho la kimataifa, ndio bima ya maisha yake.

Awali Rais Maduro alikuwa ametangaza kwamba Guaido angelikamatwa kwa kuondoka nchini kinyume na sheria na kwa kuitisha uasi dhidi ya taifa lake. Masuala yake ya kifedha pia yanachunguzwa.

Hadi muda mchache uliopita, Maduro alikuwa ana njia zake za kuwazuwia wanasiasa wa upinzani wanaoungwa mkono na umma au kuwazuwia kugombea kabisa kabisa. Muhimili wa mahakama bado unaendelea kumuunga mkono yeye.

Thofern Uta Kommentarbild App
Na Uta Thofern

Ukweli kwamba Guaido bado anaweza kuendesha gari yake kwa furaha ndani ya mji mkuu na kutangaza maandamano mbele ya maelfu ya wafuasi wake kwa sasa ndiyo ishara pekee kuwa Maduro analo jambo analingojea.

Nguvu kubwa kutoka nje?

Mataifa yanayomuunga mkono mtu huyu aliyejitangaza kuwa rais wa mpito, hasa Marekani na Umoja wa Ulaya, yalishaweka wazi kwamba kumkamata Guaido kutakuwa na matokeo mabaya kwa Maduro. Lakini ubaya wa matokeo hayo bado haujawekwa wazi.

Marekani bado haijaondosha uwezekano wa kuingilia kijeshi, ingawa linaonekana jambo lisilowezekana. Hatua kama kama hiyo haitaunganisha nchi hiyo iliyogawanyika, itaudhuru upinzani wenyewe kwa muda mrefu ujao na inaweza pia kukataliwa na mataifa jirani ambayo sasa hivi yanamuunga mkono Guaido.

Bado kanda hiyo inaamini kwenye dhana ya uovu wa ubeberu wa Kimarekani na uingiliaji kati wake. Kwa miongo kadhaa, Cuba imeijenga dhana hiyo na kuaminika, na kwa msaada wa Urusi na Venezuela yenyewe.
 
Kwa upande mwengine, ni vigumu pia kuendelea kuongeza vikwazo bila ya kuwaumiza wananchi wa kawaida wasiokuwa na hatia. Tayari Marekani imeshatumia silaha yake kubwa kabisa kwa vikwazo dhidi ya sekta ya mafuta, sasa vikwazo vinavyoweza kuwekwa ni dhidi ya watu mmoja mmoja tu. 

Lakini suala kubwa kwenye mchezo huu wa kuviziana hadi sasa ni hili: itauchukuwa utawala wa Maduro muda gani kumalizikiwa na fedha za mafuta na kwa umbali gani mvuto alionao Guaido utawabakisha wafuasi wake wakimuunga mkono!

Chanzo: Uta Thofern/DW